Tanzania sasa yapata fursa ujenzi wa viwanda vya dawa

Muktasari:

Mkutano wa mawaziri wa afya na wanaohusika na masuala ya Ukimwi hivi karibuni ulipitisha uteuzi wa Tanzania kuwa mnunuzi wa dawa kwa nchi 15 wanachama wa Sadc.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu amesema hatua ya Tanzania kuteuliwa kuwa mnunuzi wa dawa wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) itatoa fursa mpya ya ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaatiba nchini.

Mkutano wa mawaziri wa afya na wanaohusika na masuala ya Ukimwi hivi karibuni ulipitisha uteuzi wa Tanzania kuwa mnunuzi wa dawa kwa nchi 15 wanachama wa Sadc.

Akizungumza na gazeti hili juzi katika mahojiano maalumu, Bwanakunu alisema hatua hiyo ni fursa mpya kwa Watanzania kuwekeza kwenye viwanda vya dawa na vifaatiba kwa sababu ya uhakika wa soko.

“Watanzania wajipange kuuza vifaa tiba kama vile pamba, bandeji na hata maji ya dripu. Tanzania haiwezi kuwa kituo halafu ishindwe kuwapa tenda wazabuni wanaokidhi vigezo wa hapa nyumbani,” alisema.

Bwanakunu alisema si lazima kuwekeza kwenye viwanda vya kitaalamu isipokuwa kwenye bidhaa za vifaa tiba jambo linalowezekana.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa vifaa vingi vya tiba vimekuwa vikiagizwa nje ya nchi kutokana na kukosekana viwanda vinavyoweza kukidhi vigezo na kupewa tenda ya kutosheleza mahitaji hata yale ya ndani ya nchi.

“Niliwahi kutafuta kiwanda kwa ajili ya kununua peni za kusambaza kwenye vituo vya afya, hakuna ilibidi tuagize nje ya nchi. Kama kipo waje wanione tuwape biashara,” alisema.

Bwanakunu alisema hata maji ya dripu kwa sasa yananunuliwa Uganda jambo alilosema ni la aibu kwa kuwa yangeweza kutengenezwa nchini.

Alisema nchi yoyote inayotaka kuendelea lazima iwe na viwanda na ni jukumu la MSD na Serikali kufanya uwekezaji kwenye viwanda kwa vitendo.

Bwanakunu alisema MSD imetoa zabuni kwa viwanda vya ndani vilivyopo na zaidi ya Sh20 bilioni zimeshalipwa kwa wamiliki wake.

Alisema Tanzania ina viwanda vitano vya dawa vinavyofanya kazi na vingine vingi vinaanzishwa.

Bwanakunu alisema fedha inayozunguka kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa ni zaidi ya Sh1.3 trilioni kwa maana ya Serikali, wafadhili, bima ya afya, wananchi na vyanzo vingine.

Akizungumzia namna MSD itakavyofanya kazi, Bwanakunu alisema itaweka kitengo maalumu ambacho kitakuwa kinashughulikia ununuzi wa dawa, vifaatiba na vitendanishi vya maabara kupitia mfumo wa ununuzi shirikishi.

Bwanakunu alisema hatua hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa bei ya dawa na vifaatiba kwa ajili ya matumizi ya nchi wanachama wa Sadc.

Akizungumzia malalamiko kuhusu upungufu wa dawa, alisema MSD inazo za kutosha na kwamba, mwaka wa fedha ulioisha Serikali ilitoa asilimia 100 ya fedha zote za dawa zilizohitajika.

Alisema aina 135 za dawa muhimu zisizopaswa kukosekana kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini zikiwamo zahanati na vituo vya afya, zinapatikana.

Bwanakunu alisema malalamiko mengi hutokana na uelewa wa mtu mwenyewe baada ya kuandikiwa dawa ambazo akienda dirishani huzikosa kwa kuwa si zinazonunuliwa na Serikali; kutofautiana kwa magonjwa au oda ya vituo vya kutolea huduma kucheleweshwa.

Alisema Wizara ya Afya hupeleka fedha kwa wahusika wanaotoa huduma za afya na wao hutakiwa kuagiza dawa MSD kulingana na mahitaji yao.