Upinzani unavyoyumba baada ya kuisha uchaguzi

Muktasari:

Na migogoro hiyo, ambayo baadhi hutokana na usaliti, ni moja ya sababu zinazofanya vyama hivyo kusambaratika hasa baada ya Uchaguzi Mkuu, kwa mujibu wa wachambuzi.

Dar es Salaam. Mgogoro unaoonekana kukiandama Chama cha Wananchi (CUF) si wa kwanza kutokea; kila Uchaguzi Mkuu unapoisha vyama vya upinzani huingia kwenye migogoro ambayo wakati mwingine huvidhoofisha, gazeti la Mwananchi linaweza kukuhakikishia.

Na migogoro hiyo, ambayo baadhi hutokana na usaliti, ni moja ya sababu zinazofanya vyama hivyo kusambaratika hasa baada ya Uchaguzi Mkuu, kwa mujibu wa wachambuzi.

CUF iko kwenye mgogoro wa kiuongozi unaotishia uhai wa chama hicho baada ya kundi moja kutokubaliana na kitendo cha Profesa Ibrahim Lipumba kurejea madarakani baada ya kutangaza kujiuzulu kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita na jingine likiafiki barua yake ya kubatilisha uamuzi huo aliyoandika takriban mwaka mmoja baadaye.

Tangu siasa za ushindani ziliporejeshwa mwaka 1992, hali hiyo imekuwa ikijitokeza kila baada ya Uchaguzi Mkuu, kuanzia ule wa mwaka 1995 hadi wa mwaka jana.

“Sababu kubwa inayofanya vyama vingi vya upinzani kufa baada ya uchaguzi ni mfumo mbovu wa kiuongozi. Wengi huingia (vyama vya upinzani) kwa nia ya harakati na si kuongoza,” alisema mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na mbunge wa Jimbo la Donge, Sadifa Juma.

“Vyama vingi vya upinzani havina viongozi tangu ngazi ya matawi, hivyo baada ya uchaguzi, viongozi wa juu huwa hawawezi kwenda ngazi za chini na hivyo, chama kinabaki juu ambako ukiibuka mgogoro wowote hata mdogo lazima kimomonyoke.”

Alisema misingi ya vyama vya upinzani ya kupata uongozi inachangia zaidi kusambaratika, tofauti na CCM ambao huanza uchaguzi tangu ngazi ya matawi, kwa kufuata katiba yao.

Maoni yake yanapingana na ya mchambuzi wa siasa, Julius Mtatiro, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya CUF inayopingwa na kundi linalomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba.

Mtatiro alisema zipo dalili za hujuma zinazochangia vyama vya upinzani kuyumba na pengine kusambaratika.

“Mfano CUF ilivyokuja nguvu kubwa ya Ukawa, kina Lipumba walizunguka na kutangaza kuwa hiyo ndio njia ya kuingia madarakani. Mpaka dakika ya mwisho tunataka kwenda kwenye uchaguzi tuliona wao wakijiuzulu na kusema watakuja kusaidia Serikali ijayo, sasa tena wanataka kurudi madarakani,” alisema Mtatiro.

“Huu ni wakati ambao hujuma kwa chama lazima ziwe kubwa.”

Mtatiro alisema migogoro mingi kwenye vyama vya siasa vya upinzani huwa inapandikizwa ili visifanikiwe kuingia madarakani, jambo ambalo alisema huviathiri kwa muda mrefu.

Hata hivyo, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Profesa Mwesiga Baregu alisema migogoro ndani ya vyama ni dalili za kukua na kwamba, hakuna mafanikio bila kupitia kwenye changamoto hizo.

“Ukiangalia uzoefu wa kufanya siasa, kimsingi vyama vya upinzani ni vichanga, vipo katika kipindi cha mpito na vinakuwa haraka sana kwa maana ya wanachama, ikiwamo kupokea (wengine) toka chama tawala,” alisema Profesa Baregu.

“Changamoto za kukua ndizo zinazofanya vyama kuingia kwenye migogoro. Kwa maana nyingine, migogoro ni njia ya kufanikiwa.”

Profesa Baregu, ambaye sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na ambaye alishuhudia wakati NCCR ikiingia kwenye mgogoro baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1995, alisema kitendo cha kupokea wanachama wengi, wakiwamo wale wanaopigana vikumbo kutaka waingie madarakani husababisha kuwapo kwa migogoro ambayo bila hiyo kuwapo, vyama vya upinzani havina uhai.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Sanga amevitaka vyama vya siasa kuandaa misingi mizuri ya upatikanaji wa uongozi ili visiyumbe baada ya chaguzi hata kama kutakuwa na hujuma.

“Wakiwa na katiba zinazowawezesha kupata uongozi, hawatahangaika. Kinachowatesa kuna baadhi yao wanamiliki nafasi zao. Wenyeviti wanaona ni haki yao kubaki kwenye nafasi hiyo milele. Sasa hali ikiwa hivyo na ikatokea hujuma lazima chama kiyumbe,” alisema.

Baada ya Profesa Lipumba kukaa nje ya CUF kwa takriban mwaka mmoja, aliandika barua ya kufuta uamuzi wake na kutaka arejee kwenye nafasi yake ya uenyekiti, lakini mkutano mkuu ulipoitishwa ulikubaliana na barua yake ya kujiuzulu.

Wakati mkutano huo ukijiandaa kwa hatua ya pili ya kuchagua mwenyekiti, ulivunjika kutokana na vurugu za wanachama na kusababisha ajenda hiyo kuahirishwa.

Tangu hapo kumekuwa na makundi mawili, moja likifanya kazi zake kutokea Zanzibar na jingine kutokea Buguruni na juhudi za kutaka Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, ziiishia kwa kueleza kuwa anamtambua Profesa Lipumba.

Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye amekuwa akigombea urais tangu mwaka 1995 alijiondoa kwenye uenyekiti akidai dhamira inamshtaki baada ya chama hicho kuwa katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliokubaliana kumsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea urais.

Awali, Lipumba ndiye aliyeshiriki mchakato wa kumpokea Lowassa kutoka CCM na kuingia umoja huo unaoundwa pia na Chadema, NLD na NCCR-Mageuzi.

Mbali na Lipumba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa naye alijivua nafasi yake kipindi hicho, akilalamikia hatua hiyo.

Tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urejeshwe mwaka 1992 na hatimate uchaguzi mkuu wa kwanza kufanyika mwaka 1995, kumekuwa na tabia ya kupanda na kushuka kwa vyama hivyo baada ya uchaguzi.

Mwaka 1995, CCM ilipata upinzani mkali kutoka kwa NCCR Mageuzi kilichompokea Augustine Mrema kutoka CCM na kumpa uenyekiti na baadaye kumpa fursa ya kugombea urais.

Mrema, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, alijitoa CCM baada ya kuhamishiwa Wizara ya Kazi na Ajira na kuondolewa nafasi hiyo.

Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 1995, mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa akipigiwa debe na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alipata kura 4,026,422 (sawa na asilimia 61.82), wakati Mrema alipata kura 1,808,616 (asilimia 27.77) ya wapiga kura 6,846,681 waliojiandikisha.

Baada ya uchaguzi huo, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Temeke Ramadhani Kihiyo alienguliwa mwaka 1998 na hivyo kufanyika uchaguzi mdogo na Mrema aligombea na kushinda, hata hivyo hakufaidi nafasi hiyo baada ya mzozo kuibuka NCCR kati ya kambi za Mrema na katibu wake Mabere Marando kila upande ukikosoana kwa kukihujumu chama.

Hatimaye mwaka 1999, Mrema aliamua kujiengua na kundi kubwa na kuhamia TLP anayoiongoza hadi sasa.

Baada ya kuondoka kwa Mrema, NCCR Mageuzi ilidhoofika na kufanya vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Wakati NCCR ikishuka, nguvu ya CUF iliongezeka na mwaka 2005 chama hicho kilijikuta katika wakati mgumu dhidi ya Jeshi la Polisi.

Mgombea urais wa CUF katika uchaguzi uliofuata, Profesa Lipumba alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2000 na 2005 kabla ya Chadema kumsimamisha Dk Slaa mwaka 2010 aliyeshika nafasi ya pili.

Lakini migogoro haikuviandama vyama hivyo. TLP iliingia kwenye mgogoro ambao hata hivyo haukuja baada ya uchaguzi, bali kabla ya uchaguzi.

Mrema aliingia kwenye malumbano na mbunge wa zamani wa Kerwa kwa tiketi ya chama hicho, Benedict Ntungirei, aliyetangaza kugombea uenyekiti wa TLP mwaka 2009. Mbunge huyo wa zamani aliingia CCM mwaka 2000 na kugombea ubunge, akishinda katika kura za maoni na baadaye kuenguliwa.

Mwaka juzi alijiunga na Chadema. Chadema, ambayo imekuwa ikionekana kuongezeka nguvu, pia haikupona katika migogoro hiyo. Mgogoro wake uliibuka miaka miwili baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 wakati mmoja wa wabunge wake waliopata umaarufu mkubwa bungeni, Zitto Kabwe alipotaka kugombea uenyekiti.

Zitto pamoja na wanachama wengine, walichukuliwa kuwa ni wasaliti na baadaye chama kikatangaza kuwavua uanachama, lakini haukuathiri ubunge wa Zitto hadi mwaka 2015 wakati Mahakama Kuu ilipotoa uamuzi.

Mgogoro huo ulikiyumbisha chama hicho ambacho kwa sasa ndicho kikuu cha upinzani.