Utingo ajeruhiwa, magari saba yakiteketea Rusumo

Ngara. Idadi ya magari yaliyoteketea kwa moto katika kituo cha forodha Rusumo Wilaya ya Ngara mkoani Kagera mpakani mwa Tanzania na Rwanda, imeongezeka na kufikia saba na trekta moja huku utingo wa moja ya gari hayo akipelekwa hospitalini baada ya kujeruhiwa.

 

Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mntenjele amesema tukio limetokea leo Agosti 19, 2018.

 

Kanali Mtenjele amesema utingo wa gari lililokuwa limebeba petroli alibahatika kuruka na kuumia na amepelekwa Hospitali ya Nyamiaga kwa matibabu, huku eneo la tukio likiwa limetanda taharuki kutokana na ukosefu wa gari la zimamoto.

"Tumewasiliana na viongozi wenzetu wa nchi jirani ya Rwanda wameahidi kutuma helikopta ya kuzima moto na kuokoa mali za wananchi na maisha yao," amesema.

 

Amesema kukosekana kwa gari la zimamoto wilayani Ngara hasa kata hiyo ya Rusumo ni changamoto kubwa katika kuokoa maisha ya wananchi na mali zao.

Wakala wa forodha kituo cha Rusumo, Abdul Shakuru alisema gari lililosabanisha ajali ni mali ya kampuni ya Lake Oil na magari mengine ni ya kampuni ya Azam  ambayo hufanya shughuli zake za kusafirisha mizigo kutoka Tanzania kwenda Rwanda.

Amesema takriban magari 60 yaliyokuwapo na kwamba, kwa siku yanapita zaidi ya 80 mpaka 100 yanayosafirisha mizigo kwenda Rwanda na DRC Kongo, huku mengine yakirejea Dar es Salaam.

 

Shakuru amesema licha ya vituo vya forodha kufanya kazi saa 24 kwa Tanzania na Rwanda, changamoto upande wa Ngara hakuna maegesho ya uhakika na tukio hili la kuteketea magari liinaweza kuwa sita kwa miaka mitatu iliyopita. 

 

Eneo palipotokea ajali hiyo ni umbali wa kilomita 40 kutoka Rusumo hadi makao makuu ya Ngara na kilomita tatu kuingia kituo cha forodha upande wa Rwanda, zikiwa ni kilomita 130 kutoka Rusumo kwenda Karagwe ambako kuna gari la zimamoto.