Vigogo wawili Acacia wadakwa na Takukuru

Deo Mwanyika

Muktasari:

  • Vigogo hao, Mwanyika na Lugendo walikamatwa na Takukuru kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.



Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemkamata aliyekuwa makamu wa rais wa kampuni ya Acacia, Deo Mwanyika na Alex Lugendo ambaye ni mshauri wa Serikali ndani ya kampuni hiyo ya uchimbaji madini.

Mwanyika aliyejiunga na Acacia mwaka 2001 akiwa ameitumikia kampuni hiyo kwa nafasi mbalimbali kwa miaka 17, alitangazwa kujiuzulu Agosti 24 kwa barua ya ofisa mtendaji mkuu wa Acacia, Peter Galeta kwenda kwa wafanyakazi wote wa kampuni hiyo.

Akizungumza na Mwananchi jana, naibu mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema wanawashikilia wawili hao tangu juzi na leo wanaweza kufikisha mahakamani kwa hatua zaidi.

“Tumewakamata kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi katika tasnia ya madini,” alisema Mbungo.

“Lakini hawa wakiwa viongozi waandamizi walishindwa kusimamia nchi ipate mapato kama ilivyotakiwa.”

Naibu mkurugenzi huyo alisema wamefanya mahojiano na watuhumiwa hao kwa kipindi kirefu.

“Baada ya kukamilisha mahojiano tangu tulipowakamata jana (juzi), leo (jana) tuliwapeleka mahakamani lakini kutokana na sababu zilizojitokeza walishindwa kupandishwa kizimbani lakini kesho (leo) natarajia itawezekana,” alisema.