Wabunge wa Chadema waliomba Jeshi la Polisi liwasaidie

Muktasari:

Wabunge hao wameomba msaada huyo baada ya mawakala wao kudaiwa ‘kutekwa’

Arusha. Wabunge wa Chadema wameliomba Jeshi la Polisi  kudhibiti kamata ya wafuasi wa chama hicho wakiwemo mawakala ‘wanaotekwa’ vituoni.

Mbunge wa Monduli(Chadema), Julius Kalanga akizungumza na Mwananchi leo Jumapili amesema hadi sasa  vijana wanne wamekamatwa huku wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM wakiwa wamezingira vituo vya kura.

"Hapa Kata ya Moita wamekamata vijana, CCM wamekaa vituoni wanalazimisha wasiojua kusoma wao ndio wawapigie kura na polisi wameshindwa kuwadhibiti," amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum(Chadema) Arusha, Cesilia Pareso anasema Kata ya Embuleni mawakala wametekwa na jitihada kuwasaka zimekwama.

Alipoulizwa kuhusu hali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha  Charles Mkumbo  amesema wanafuatilia vurugu maeneo mbalimbali na atatoa taarifa rasmi.

"Tunapokea taarifa za vyama na tunafanyia kazi na tutatoa taarifa," amesema.