Wabunge Kubenea, Komu kusuka au kunyoa leo

Muktasari:

  • Hatima ya wabunge wawili wa Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) itajulikana leo wakati uongozi wa Chadema utakapoeleza maazimio ya kikao cha Kamati Kuu kilichoketi jana kuwahoji wabunge hao.

Dar es Salaam. Hatima ya wabunge wawili wa Chadema, Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) itajulikana leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 saa 5 asubuhi wakati uongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania utakapoeleza maazimio ya kikao chake cha Kamati Kuu kilichoketi jana kuwahoji wabunge hao.

Kikao hicho cha dharura kilifanyika jana Jumatano katika Hoteli ya Bahari Beach kikiwa na ajenda moja ya kuwajadili wabunge hao.

Kubenea na Komu katika siku za hivi karibuni wamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa kuwa ni sauti yao iliyokuwa ikisikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamekana kuhusika na sauti hizo kwa kile walichoeleza ni za kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama.

Jana, baada ya Komu kumaliza kuhojiwa na kumpisha Kubenea, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema alisema leo saa 5 asubuhi watatoa maazimio ya kikao hicho.

“Leo saa tano makao makuu ya chama tutaeleza maazimio ya chama. Siwezi kuyasema kwa sasa ila subiri muda ukifika,” amesema Mrema.

“Kwa sasa taarifa itakayosomwa mbele ya wanahabari ndiyo inaandaliwa, usiwe na haraka sasa subiri mwenyewe utasikia na kuona.”

Jana, wabunge hao waligoma kuzungumzia walichohojiwa wakieleza kuwa hawapaswi kufanya hivyo.

Endelea kufuatilia MCL Digital itarusha moja kwa moja mkutano huo kati ya uongozi wa Chadema na waandishi wa habari.