Wabunge wataka ulinzi, Serikali yaweka ngumu

KUSHAMBULIWA KWA LISSU, WABUNGE WATAKA ULINZI

Muktasari:

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo bungeni mjini Dodoma jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Adadi Rajab alisema ulinzi huo uwe katika makazi ya wabunge wakiwa wanatekeleza majukumu ya kibunge mjini Dodoma na katika majimbo yao.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imependekeza kufanyiwa marekebisho Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kuweka sharti la wabunge kupatiwa ulinzi katika maeneo mbalimbali.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo bungeni mjini Dodoma jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Adadi Rajab alisema ulinzi huo uwe katika makazi ya wabunge wakiwa wanatekeleza majukumu ya kibunge mjini Dodoma na katika majimbo yao.

Mapendekezo ya kamati hiyo yalionekana kuwagusa wabunge wengi baada ya mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa wakati akichangia taarifa hiyo ya kamati kutoa mfano wa tukio la kupigwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na hivyo kupendekeza wabunge walindwe.

Si Mwambalaswa tu, kwani mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye naye aliitaka Serikali kupeleka bungeni Sheria ya Usalama wa Taifa ili ifanyiwe marekebisho kwa madai kuwa haitoi nafasi ya kuwalinda raia na badala yake inazungumzia ulinzi wa viongozi pekee.

Wakati Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akiiagiza Serikali kulifanyia kazi suala la ulinzi na uwekaji wa namba maalumu kwa magari ya wabunge kama ilivyopendekezwa na kamati, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika walipangua baadhi ya mapendekezo ya kamati na wabunge.

Lissu alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana na kisha kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na siku hiyo hiyo usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya ambako alitibiwa kwa siku 121 kabla ya Januari 6 kuhamishiwa Ubelgiji kwa ajili ya mazoezi zaidi.

Suala la Lissu pia liliibuliwa bungeni juzi jioni na mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliyehoji sababu za mbunge huyo kutibiwa kwa michango ya wananchi huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akitibiwa nje ya nchi wa gharama za Bunge.

Taarifa ya kamati

Akiwasilisha taarifa hiyo, Balozi Rajab alisema kamati imependekeza pia kuweka utaratibu wa kutoa namba maalumu za usajili wa magari ya wabunge.

Alisema hakuna sheria wala kanuni inayoelekeza wabunge kupewa ulinzi katika makazi yao na hivyo kuliacha suala la ulinzi na usalama kuwa jukumu binafsi.

“Kazi ya wabunge ni kuisimamia Serikali, zinagusa maslahi ya watu au makundi binafsi ambayo yanaweza kujenga chuki dhidi yao,” alisema mbunge huyo wa Muheza.

Pia aliitaka Serikali kuboresha na kuimarisha ulinzi katika maeneo ya magari bungeni.

Aliwataja viongozi wanaolindwa kwa sasa kuwa ni Rais, Makamu wa Rais, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri Mkuu, viongozi wastaafu, mawaziri na manaibu mawaziri, wakuu wa wilaya na mikoa, Spika wa Bunge na Naibu Spika.

Kuhusu ulinzi na usalama wa raia na mali zao, Rajab alisema matukio yanayohatarisha hali ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao yamekuwa yakijirudiarudia na hivyo kujenga hofu miongoni mwa wananchi.

Alisema taarifa na hatua zilizofikiwa katika upelelezi wa matukio hayo zimekuwa hazitolewi mara kwa mara kwa umma na hivyo kusababisha wananchi kutofahamu hatua zilizofikiwa.

“Jeshi la Polisi liwe na utaratibu wa kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu zilipofikia katika upelelezi wa matukio ya muda mrefu ambayo yamevuta hisia za jamii kama vile mauaji na kupotea kwa wananchi mbalimbali,” alisema.

Aliyataja matukio hayo kuwa ni mauaji, kutekwa na kupotea kwa viongozi na wananchi mbalimbali, unyang’anyi kwa kutumia silaha na makosa makubwa ya uhujumu uchumi.

Alisema kamati hiyo imeridhishwa na juhudi za Serikali katika kushughulikia matukio mbalimbali ya uhalifu hususani ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji ambayo yalihusisha mauaji ya viongozi kadhaa.

Wabunge wafunguka

Wakichangia taarifa ya kamati hiyo pamoja na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Mwambalaswa alisema hali ilipofikia kwa sasa si nzuri kwa sababu Taifa linapitia katika kipindi kigumu.

Mwambalaswa alisema bila ya wabunge kupewa ulinzi wataendelea kuwa katika hofu na mashaka katika baadhi ya maeneo wanayoishi na utendaji kazi wao utakuwa shakani.

“Mbunge mwenzetu alipigwa risasi hapa Dodoma (Lissu), pia Meja Mstaafu wa Jeshi alipigwa risasi lakini bado tunaendelea kuona matukio mengi ya ajabu yanaendelea katika nchi yetu, je tunataka nini kifanyike,” alihoji mbunge huyo wa Lupa.

Mbunge huyo alitaja sababu tatu kubwa ambazo zinafanya usalama wa watu kuwa shakani kuwa ni; utandawazi, ukosefu wa ajira kwa vijana na hali tete za usalama katika nchi jirani na Tanzania.

Alipendekeza wabunge walindwe hata wanapokuwa majimboni mwao au kuwekewa magari maalumu yenye namba za utambulisho, lakini wanapokuwa Dodoma waishi sehemu moja kuimarishiwa ulinzi.

Nape akichangia hilo alisema, “Vita ya kiuchumi ambayo imeanzishwa na Rais John Magufuli ni nzuri sana na inafaa kupongezwa lakini inaweza kukosa maana yoyote ikiwa sheria ya usalama wa taifa itabaki kama ilivyo.

“Sheria ilivyokaa inaonyesha wazi kuwa imetungwa kwa kuwapa nafasi Usalama wa Taifa kuwalinda viongozi, lakini siyo kuwalinda wananchi na ndiyo maana kila siku tunapigwa katika miradi mbalimbali kama Epa, Escrow na maeneo mengine.”

Waziri huyo wa zamani wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo aliwaomba Watanzania kutolaumu Usalama wa Taifa kwa sababu wamefungwa mikono na sheria hiyo na akaonya kuwa hali itaendelea kuwa mbaya kama sheria hizo hazitafanyiwa kazi.

Alisema taasisi hiyo ingekuwa na mlengo wa kuwalinda wananchi hakuna jambo ambalo lingefanyika kinyume, na kauli ya siasa ni uchumi ingekuwa na maana kubwa sana.

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa aliitaka Serikali kuondoa usiri wa bajeti ya Usalama wa Taifa ili wabunge wajue kiasi kinachopelekwa huko ingawa siyo lazima kujua matumizi yake.

Msigwa alisema Usalama wa Taifa unatumiwa kama kivuli cha kujificha, lakini kuna watu ambao wanakula mabilioni ya fedha ikiwemo ubadhirifu wa miradi kama hati za kusafiria.

Waziri Mwigulu ajibu

Akijibu hoja za wabunge hao, Mwigulu alisema, “Hoja ya kuwalinda wabunge mmoja mmoja itakuwa ni ngumu kutokana na ukweli kuwa miundombinu ya taifa haijaruhusu kufikia hatua hiyo.”

Alisema ulinzi kwa mbunge mmoja mmoja unaweza kuhatarisha hata usalama wa askari kwani watu wenye nia mbaya wanaweza kuwatafuta kwa lengo la kutaka kuwapora silaha.

Alisema katika mataifa mengine ambayo wabunge wanalindwa jambo hilo hufanyika kirahisi kwa kuwa huwa wanachaguliwa eneo moja la kuishi.

Mchungaji Msigwa abanwa

Kuhusu ufisadi katika hati za kusafiria, Dk Tulia alimzuia Mwigulu kujibu kwa maelezo kuwa tayari ameiagiza kamati ya maadili kumuita Mchungaji Msigwa ili awasilishe ushahidi wake.

Wakati akichangia taarifa hiyo, Mchungaji Msigwa alisema mradi wa hati za kusafiria umelitia Taifa hasara kwa kiasi kikubwa na akabainisha kuwa ana ushahidi wa wazi.

Dk Tulia alimtaka kuupeleka ushahidi katika kamati hiyo kwa kuwa alilieleza Bunge kuwa anao na akafafanua kuwa anafanya hivyo kwa ajili ya kukidhi matakwa ya kanuni ya 63 kuhusu mbunge kusema uongo bungeni.

Mkuchika na Usalama wa Taifa

Mkuchika alisema Usalama wa Taifa wanabebeshwa mzigo na lawama za bure kwa maelezo kuwa kuna baadhi ya maeneo hawahusiki. “Kazi ya Usalama wa Taifa hamuijui maana kama mngeijua msingesema hapa hadharani, lakini kuna mambo mengine ambayo mnawatwisha usalama lamawa za bure,” alisema Mkuchika.

Alipinga lawama zinazoelekezwa kwa chombo hicho kwa kuhusishwa na matukio mengi ya kupotea kwa watu akisema mambo hayo yanatakiwa kuelekezwa kwa Polisi kwani usalama wanafanya mambo yao kwa taratibu na kuishauri Serikali.

Lema na Lissu

Juzi wakati akichangia taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati za Bunge za Utawala na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria na Sheria Ndogo, Lema alisema, “Mheshimiwa Spika anatumia fedha za Serikali kupata matibabu na Mbunge Lissu tumeendelea kumtafutia fedha za matibabu mitaani tena kwa mkopo.”

Alibainisha kuwa kitendo cha Ndugai kutibiwa na fedha za Serikali huku Lissu ambaye ni mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni akishindwa kupewa msaada na Bunge ni jambo ambalo halikubaliki.

Wakati akieleza hayo, alikatishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akimtaka ajielekeze kwenye hoja tatu za taarifa za kamati huku mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi akisema bima walizonazo wabunge zinawawezesha kupata matibabu.

Kauli ya Nchambi iliibua mvutano bungeni, huku mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche akisikika akisema kauli ya mbunge huyo wa Kishapu ni sawa na kucheza na uhai wa mtu.

Kufuatia hali hiyo, Chenge aliingilia kati na kuwatuliza wabunge hao kwa kuwataja kwa majina, akiwemo Heche na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Licha ya Lema kuendelea kuchangia taarifa hizo za kamati huku akikatishwa mara kwa mara, muda wake ulipomalizika alitakiwa na Chenge kuketi ili kumpisha mchangiaji mwingine.