Wanafunzi wamkumbuka Idrissa aliyetekwa ‘kimafia’

Muktasari:

  • Septemba 26 Idrissa, alichukuliwa na dereva mwanaume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST, ambaye baada ya kuwafukuza marafiki zake Idrissa alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo hatimaye kumuingiza mlango wa nyuma wa gari lake.

Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi wanaosoma shule moja na Idrissa Ally (13) aliyetekwa staili ya kimafia na mtu asiyejulikana siku sita zilizopita wamesema wanajiona wapweke na wanyonge kwa mwanafunzi mwenzao kutoonekana mpaka jana.

Idrissa anayesoma darasa la tano Shule ya Msingi Princes Gate alitekwa Jumatano iliyopita Septemba 26 saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti jijini Dar es Salaam.

Wanafunzi hao wanaosoma darasa moja na Idrissa la wanafunzi 17 na sasa wamebaki 16 walieleza hayo jana wakati wakizungumza na Mwananchi shuleni hapo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake kwa sauti ya chini na yenye majonzi, Imran Othman alisema wamemkumba rafiki yao kwa jinsi walivyokuwa wakiishi naye wakiwa shuleni hapo hususan darasani.

“Idrissa ni mcheshi, asiyependa kugombana na mwanafunzi mwenzake, ni rafiki wa kila mmoja. Tumemkumbuka sana, tunajisikia vibaya kutomuona kwa siku hizi.”

“Tunaiomba Serikali itusaidie apatikane,” alisema Othman ambaye wakati anazungumza kichwa chake alikuwa amekiinamisha huku akichezea mikono yake

“Mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa Jumanne, aliniomba niende kwao, nikamweleza amwambie mama yake aje kuomba ruhusa shule ili niende,” alisema Othman akiwa mwenye huzuni.

Othman aliungwa mkono na Atuiya Salehe ambaye alisema wapo kwenye upweke baada ya kutomuona Idrissa kwa siku sita na walistuka walipopata taarifa kuwa kachukuliwa na wanaendelea kumuomba Mungu ili aliyemchukua Idrissa amrudishe akiwa salama.

“Tunajisikia upweke kutokuwepo kwa Idrissa hapa shuleni. Mara ya mwisho kuongea naye nilimuomba kitabu cha sayansi akanijibu kuwa hana, nimemkumbuka mwanafunzi mwenzetu,” alisema Atuiya.

Wanafunzi hao, walizungumza na Mwananchi baada ya mwalimu mkuu wa shule hiyo, Mussa Idrissa kusema kwamba wapo pamoja na familia ya kina Idrissa katika jitihada za kumtafuta.

“Kila siku naenda kwa kina Idrissa mara mbili asubuhi na jioni, kujua familia ilipofikia na walimu tulipofikia katika kumtafuta Idrissa,’’ alisema.

Mama mzazi wa Idrissa, Leila Kombe huku akitokwa machozi alisema hawezi kuongea mengi kwa sasa zaidi ya kumuomba Mungu mwanaye arudi.