Wananchi fanyeni kazi, sitatoa chakula cha bure – Rais Magufuli

Muktasari:

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Septemba 9, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Simiyu akitokea Mara.

Rais John Magufulia amewaambia wakazi wa Itilima mkoani Simiyu wachape kazi, huku akisisitiza kuwa Serikali haitatoa chakula cha bure.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Septemba 9, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Simiyu akitokea Mara.

Amewataka wananchi hao kutafuta maendeleo ya kweli hasa kwenye kilimo ambacho ndiyo shughuli kuu ya uchumi wao.

“Endeleeni kuchapa kazi, chakula cha bure hakitakuja. Hili lazima niwaambie ukweli, Serikali haina shamba,”  amesema Rais Magufuli aliposimama na kuzungumza na wakazi hao.

Rais Magufuli amewataka pia kuachana na imani za kishirikina badala yake wapeleke watoto wao shule kwa sababu Serikali inatoa elimu bure.

“Kila mwezi tunatoa Sh23.85 bilioni kwa ajili ya elimu bure. Pelekeni watoto shule,” amesema Magufuli huku akishangiliwa na wananchi hao.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli ameambataka na mawaziri watano ambao ni Seleman Jafo (Tamisemi), Profesa Makame Mbarawa (Maji na Umwagiliaji), Ummy Mwalimu (Afya), Kangi Lugopa (Mambo ya Ndani) na Mhandisi Isaac Kamwelwe (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano).

Rais aliwapa mawaziri hao nafasi ya kusalimia wananchi ambao kila mmoja alitumia nafasi hiyo kueleza mipango kazi ya wizara yake katika wilaya ya Itilima.

“Kazi ya kujenga kituo cha polisi hapa Itilima imeanza, namshukuru mbunge wa hapa, nitamwagiza IGP ili alete nguvu kazi ya kutosha kusudi wananchi hawa wawe salama wakati wote,” amesema Waziri Lugola alipopewa nafasi ya kusalimia.