Wanawake 5 wauawa kwa kuchomwa moto kwa imani za kishirikina Nzega

Muktasari:

Pia, wanafunzi wa Shule ya Msingi Undomo walirudishwa nyumbani baada ya taarifa za mauaji hayo kusambaa na kusababisha taharuki kijijini hapo.

Nzega. Idadi kubwa ya wakazi wa Kijiji cha Undomo wilayani Nzega wameyakimbia makazi yao baada ya wanawake watano kuuawa kwa kuchomwa moto kutokana na imani za kishirikina.

Pia, wanafunzi wa Shule ya Msingi Undomo walirudishwa nyumbani baada ya taarifa za mauaji hayo kusambaa na kusababisha taharuki kijijini hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mtafungwa alisema jeshi hilo litahakikisha wahusika wote wanatiwa mbaroni na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Nsuku Masali (45), Ester Kiswahili (45), Christina Said (55), Mwashi Mwanamila (50) na Kabula Kagito (60).

“Watu 51 wakiwamo viongozi wa kisiasa ngazi ya kata na kijiji wanashikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na mauaji haya,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Undomo, Paul Joseph alisema aliwarejesha nyumbani wanafunzi kutokana na hofu.

“Watoto walifika shuleni asubuhi kama kawaida, lakini nyuso zao zikiwa zimejaa hofu kiasi cha kukosa usikivu, ndipo tulipokubaliana kuwarejesha nyumbani,” alisema Mwalimu Joseph.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla ameagiza uchunguzi ufanyike ili kuchukua hatua za kisheria.

Mmoja wa wanakijiji aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema alishuhudia watu wanne kati ya hao wakipigwa hadi kufa na miili yao ikapelekwa porini na kuchomwa moto.

Mauaji hayo yanayohusishwa na imani za kishirikina, ni mwendelezo wa matukio ya kikatili katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kunakokadiriwa kuwa zaidi ya watu 20 waliouawa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Matukio hayo yanakiuka haki ya kuishi iliyoainishwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1997, sheria, matamko na mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu.