Weah asema hatapokea matokeo ya kushindwa

Muktasari:

Amesema haoni uwezekano wa yeye kushindwa kutokana na kampeni kubwa na zenye hamasa zilizofanywa na CDC.

Monrovia, Liberia. Mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani wa CDC (Coalition for Democratic Change), Seneta George Weah amesema matokeo pekee atakayoridhia kuyapokea ni yanayomtangaza kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu akidai ndiye anayelekea kushinda.

Weah, nyota huyo wa zamani wa soka aliyegeuka kuwa mwanasiasa ni kati ya wagombea 20 wanaowania nafasi ya kumrithi Ellen Johnson Sirleaf anayemaliza muda wake na ambaye hakugombea tena.

Baada ya kupiga kura yake Jumanne asubuhi kwenye kituo cha shule ya Kendja, Weah aliiambia redio Prime FM kwamba anashawishika kuamini kwamba ushindi ni wa uhakika kwa chama chake cha CDC katika uchaguzi wa mwaka huu na hakuna kitu cha kumzuia.

Alipobanwa ikiwa ataridhia matokeo ya kushindwa, Weah alisisitiza haoni uwezekano wa yeye kushindwa kutokana na kampeni kubwa na zenye hamasa zilizofanywa na CDC. Kwamba itakuwa vigumu kwake kushindwa akifafanua namna alivyowapanga mawakala wake ambao walipewa mafunzo kwa miezi miwili.

 Dosari zaibuka

Baada ya muda wa kupiga kura kumalizika wapigakura wengi waliojiandikisha walibaki wamepigwa butwaa namna walivyonyimwa haki yao na baadhi ya vyama vya siasa kama CDC na Alternative National Congress (ANC) vikiwa havina furaha kutokana na mchakato ulivyokuwa.

Wapigakura wenye shauku ya kupiga kura walianza kufika kwenye vituo saa 10:00 alfajiri wakitarajia kuwa miongoni mwa watu wa kwanza. Lakini siku iliisha vibaya baada ya baadhi yao kutoona majina yao katika Daftari la Wapigakura.