Yaliyotabiriwa na mbunge kuzama Mv Nyerere yatimia

Muktasari:

  • Mbunge huyo wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi alizungumza bungeni na kuiomba Serikali kukitazama kivuko hicho kwa jicho la pili kwa kuwa kimekuwa na matatizo, kuonya kuwa huenda kuna siku kikazama ikiwa hatua zozote hazitachukuliwa

Dar es Salaam. Unaweza kusema yaliyotabiriwa na mbunge wa Ukerewe (Chadema),  Joseph Mkundi juu ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere yametimia.

Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana mchana kivuko hicho kuzama katika Ziwa Victoria mita 50 kabla ya kutia nanga huku abiria 37 waliokuwa kwenye kivuko hicho wakifariki dunia hadi zoezi la uokoaji lilipositishwa jana jioni.

Kivuko hicho kilichokuwa kikitokea katika Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, kinadaiwa kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100, wengi wakiwa wanaelekea kwenye gulio.

Katika moja ya swali alilouliza bungeni hivi karibuni, Mkundi alitaka kupata kauli ya Serikali jinsi itakavyoshughulikia  kivuko hicho ili kisije kusababisha maafa.

Video inayomuonyesha mbunge huyo akiuliza swali hilo bungeni ilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii jana jioni baada ya kivuko hicho kuzama.

 “Naomba kupata kauli ya Serikali, ni suala ambalo tumekuwa tunalishughulikia mara kwa mara, tuna kivuko kinachounganisha Ukerewe na kisiwa cha Ukara, kivuko hiki kinahudumia watu zaidi ya 50,000,” amesema.

“Kimekuwa kinaleta shida mara kwa mara na nimekuwa nawasiliana na wizara, sipendi siku moja tuje hapa kuomba rambirambi kwa sababu ya wananchi waliozama katika kivuko kile.”