Zanzibar yahitaji madarasa 1, 200

Friday August 11 2017
ZENJI

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud

Zanzibar. Zaidi ya madarasa 1,250 yanahitajika katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ili kupunguza msongamano wa wanafunzi kusoma zaidi ya 150 ndani ya darasa moja kwa baadhi ya  shule mbalimbali ndani ya mkoa huo.

Mkuu wa mkoa huo, Ayoub Mohamed Mahmoud aliweka bayana hayo leo Ijumaa wakati akizindua kampeni za kuanza kwa ujenzi wa madarasa matatu pamoja na maktaba katika Shule ya Kijitoupele Mjini Unguja , ikiwa ni miongoni mwa kampeni maalum zinazotambulika kwa jina la ‘Mimi na Wewe’.

Alisema kuwa katika hatua za awali za kampeni hiyo wanatarajia kujenga madarasa 52, ndani ya mkoa huo, ambapo hali zaidi ya uchumi ikiridhisha ujenzi huo utandelea hatua baada ya hatua hadi kukamilika kwa madarasa yote.

“Tuna nia ya kuona ndani ya Mkoa wetu tunaitatua kero ya uhaba wa madarasa, ila kwa hatua ya awali tumedhamiria kujenga madarasa 52, yakiwemo haya matatu ya hapa, ila kila hali ya kifedha ikiruhusu tutaendelea hadi kufikia malengo ya kuona wanafunzi wanaondokana na tatizo la msongamano ndani ya darasa moja,” alisema Mahmoud.

Kamishna Mamlaka ya Bima Tanzania, Juma Makame alisema hatua ya Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa kuanzisha kampeni hiyo ya ‘Mimi na Wewe’ ni itaeleta maendeleo kwa jamii, hivyo ni vyema wanahisani na wafadhili mbalimbali kujitokeza kwa wingi katika kuunga mkono.

“Kwa upande wa mamlaka yetu tunachangia  mabati 62 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa madarasa hayo ila hatutosita kutoa ushirikiano wetu pale utakapohitajika,”alisema Makame.

Advertisement
Advertisement