Zitto, Polepole wavaana

liana jambo na Mbunge wa Mtama, Zitto Kabwe walipohudhuria kikao cha 12 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Polepole amesema madai ya Zitto kuwa kuna Sh1.5 trilioni zimepotea hayana ukweli na yanapaswa kupuuzwa, huku akizitaka mamlaka husika zimchukulie hatua mbunge huyo wa Kigoma Mjini kwa upotoshaji aliodai amekuwa akiufanya mara kwa mara kupitia matamko yake.

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole wameibua mvutano kati yao kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Polepole amesema madai ya Zitto kuwa kuna Sh1.5 trilioni zimepotea hayana ukweli na yanapaswa kupuuzwa, huku akizitaka mamlaka husika zimchukulie hatua mbunge huyo wa Kigoma Mjini kwa upotoshaji aliodai amekuwa akiufanya mara kwa mara kupitia matamko yake.

Zitto akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii akitaja ukurasa wa 34 wa ripoti ya CAG, alidai kuwa Sh1.5 trilioni hazikutolewa kwa matumizi wala kukaguliwa.

Ukurasa wa 34 wa ripoti ya CAG ya ukaguzi wa fedha za Serikali Kuu kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2017 inaonyesha kuwa kati ya Sh25,307.48 bilioni zilizokusanywa, Sh23,792.30 bilioni zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na fedha kwa ajili ya kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali pamoja na riba.

Akizungumza na Mwananchi, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi pia alipinga kauli ya Zitto akimtaka aeleze ni kwa nini chama chake hakikupeleka hesabu kwa CAG ili zikaguliwe.

“Hakuna mahali wala ukurasa wowote katika ripoti ya CAG anaposema au kuandika kuwa kuna Sh1.5 trilioni zimeibwa au kupotea. Hakuna. Watuonyeshe,” alisema Dk Abbasi.

Alisema anayetakiwa kutegua kitendawili cha fedha hizo ni CAG.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Azam hivi karibuni, CAG Profesa Mussa Assad alitaka Bunge liulizwe kuhusu fedha zilizotumika bila kuwa na maelezo kwa sababu lenyewe ndilo linasimamia utekelezwaji wa bajeti ya Serikali.

“Mimi naamini kwamba fedha hizo zimetumika katika maeneo mengine ya matumizi ya Serikali. Sasa la muhimu ni kwamba tulipanga bajeti na kazi ya Bunge ni kusimamia utekelezaji wa bajeti ile,” alisema Profesa Assad.

“Kwa sababu kama kuna ‘extra budgetary expenditure’ (matumizi ya ziada ya bajeti), sheria inataka Bunge lijulishwe liridhie,” alifafanua Profesa Assad.

Kauli ya Polepole

Polepole alisema kauli ya Zitto ni ya upotoshaji yenye lengo la kuzua taharuki kwenye jamii. “Ana bahati Rais (John) Magufuli ni mpole, vinginevyo angekamatwa kwa kupotosha ukweli na kusababisha taharuki kwenye jamii. Tunataka aeleze hiyo Sh1.5 trilioni kaipata wapi,” alisema.

Polepole alisema hakuna fedha iliyopotea akifafanua kuwa, “Makusanyo yalikuwa Sh25.3 trilioni na fedha iliyotumika ilikuwa Sh23.79 trilioni. Hiyo Sh23.7 trilioni kipindi mkaguzi anapita ilikuwepo fedha ya Serikali ambayo ilikuwa haijaiva Sh697.85 bilioni. Ukichukua hiyo Sh697.85 na kuijumlisha na Sh23.7 trilioni utapata Sh24.4 trilioni.

“Ukichukua Sh25.3 trilioni ukatoa Sh23.79 trilioni utapata Sh1.5 trilioni ambayo huyu bwana anasema imepotea, hesabu hajui amtafute mtaalamu amsaidie,” alisema.

Msimamo wa Zitto

Wakati Polepole akisema hayo, Zitto alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kujibu hoja hizo akisimamia msimamo wake kuwa hakuna maelezo kuhusu matumizi ya fedha hizo.

“Serikali ya CCM ilidhani Watanzania ni mandondocha, wanapelekwa pelekwa tu. Nimekuwa mwenyekiti wa PAC/POAC kwa miaka 8. Ninajua ninachosema. Jumla ya TZS trilioni 1.5 hazina maelezo ya matumizi yake katika mwaka 2016/17,” ameandika Zitto.

“Kuna mtu anasema nikamatwe kwa kupotosha kuhusu fedha zinazohojiwa na CAG, mimi naapa kwamba Serikali ya CCM ya awamu ya tano imeshindwa kuonyesha matumizi ya fedha hizo kwa CAG. Nipo tayari kukamatwa kwa kusema hivyo.”

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Zitto alikiri chama chake kuchelewesha hesabu zake kwa CAG kama ilivyodokezwa na Dk Abbasi lakini alisema hilo haliondoi ukweli kwamba kuna fedha hazijulikani zilikopelekwa kwenye ripoti ya CAG.

“Tumepeleka (hesabu) lakini tulichelewa. Hata hivyo, siyo hoja kabisa, hoja ni Serikali kueleza zipo wapi Sh1.5 trilioni,” alisema Zitto.