Zitto Kabwe alivyonaswa na polisi Dar

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (katikati) akitolewa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa ajili ya kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano baada ya kukamatwa jijini Dar es Salaam jana. Picha na Fortune Francis

Muktasari:

  • Fahamu 'sinema' nzima ya namna mwanasiasa huyo maarufu alivyojikuta mikononi mwa polisi akihojiwa katika vituo viwili tofauti jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Siku tatu baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuitaka Polisi kutoa maelezo ya kina kuhusu mauaji ya askari na raia mkoani Kigoma na siku moja tangu jeshi hilo kumtaka awasilishe vielelezo, limemkamata jana na kumhoji kwa saa tatu na kisha kumuweka mahabusu.

Kiongozi huyo wa Chama cha ACT-Wazalendo, alikamatwa jana saa tatu asubuhi akiwa nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay alikohojiwa kwa saa tatu kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu ambako alinyimwa dhamana.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Kijitonyama jijini hapa Jumapili iliyopita, pamoja na mambo mengine, Zitto alidai kwamba anazo taarifa za wananchi zaidi ya 100 kuuawa katika tukio la mapigano ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi katika Wilaya ya Uvinza na kutaka polisi kueleza kilichotokea.

Kauli hiyo ya Zitto ilijibiwa juzi kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno kumtaka awasilishe vielelezo juu ya kauli yake hiyo akisema tuhuma za mbunge huyo hazina ukweli wowote na kwamba ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Liberatus Sabas jana aliwaeleza wanahabari kuwa wanamshikilia Zitto kutokana na matamshi hayo.

Alivyokamatwa

Akizungumza jinsi Zitto alivyokamatwa, wakili wa mwanasiasa huyo, Jebra Kambole alisema, “Walimfuata nyumbani kwake Masaki wakamueleza kuwa wanahitaji kumhoji. Alipofika Oysterbay alitakiwa kuandika maelezo kuhusu mkutano wake na waandishi wa habari. Hiyo ilikuwa saa tano asubuhi na ilipofika saa 10 kasoro jioni wakasema wanataka kumhamishia (Central) Kituo Kikuu cha Polisi.”

Alisema alipofikishwa katika kituo hicho, waligusia suala la dhamana lakini polisi wakaeleza kuwa hawawezi kumpa dhamana kwa kuwa bado wanahitaji kuendelea kumhoji.

“Polisi wamesema hawawezi kumuachia leo, wanaendelea kumshikilia kwa ajili ya mahojiano. Wamesema hawawezi kumpa dhamana,” alisema Kambole.

katika ufafanuzi wake, Kambole alisema, “Baada ya kuhojiwa aliandika maelezo ya awali na aliwaeleza kuwa kama kuna maelezo mengine atayatoa mahakamani.

“Hakuna chochote kilichoendelea na sheria inamruhusu kama unaona hulazimiki kutoa maelezo. Maelezo kuhusu makosa yake hajayatoa na hakulazimishwa kuyatoa, anasubiri kama akipelekwa mahakamani atayatoa huko. Wamesema dhamana yake wameishikilia na kosa lake ni kutoa maneno ya kichochezi.”