Zitto ahamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi

Mbunge Zitto Kabwe akitoka kituo cha polisi cha osterbay baada ya kuhojiwa kwa masaa 3 na amehamishiwa kituo kikuu cha polis kwa mahojiano zaidi

Muktasari:

Baada ya kuhojiwa kwa saa tatu katika kutuo cha polisi Oysterbay jijini hapa, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amehamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi

Dar es Salaam. Baada ya kuhojiwa kwa saa tatu katika kutuo cha polisi Oysterbay jijini hapa, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amehamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi.

Leo Jumatano Oktoba 31, 2018 Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni lilithibitisha kumkamata mbunge huyo wa Kigoma Mjini.

Akizungumza na Mwananchi, wakili wa mwanasiasa huyo Jebra Kambole amesema baada ya mahojiano hayo, mteja wake ameelezwa kuwa anapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi.

Mwananchi limeshuhudia mbunge huyo akifikishwa kituoni hapo leo saa 10:10 jioni.

Awali, Kamanda wa polisi wa mkoa huo wa kipolisi,  Jumanne Murilo alilieleza Mwananchi kuwa mbunge huyo amekamatwa na kubainisha kuwa alikuwa akihojiwa kituo cha polisi Oysterbay.

“Ni kweli tumemkamata  tunaendelea na mahojiano naye,” amesema Murilo na alipoulizwa sababu za kumkamata amesema, “Taarifa za kina tutatoa baadaye.”

Jana, Jeshi la Polisi mkoani Kigoma lilimtaka Zitto kuwasilisha vielelezo juu ya kauli aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari Jumapili iliyopita Oktoba 28, 2018 kuwa ana taarifa za wananchi zaidi ya 100 kuuawa katika tukio la mapigano ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi wilaya ya Uvinza mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno amesema tuhuma za mbunge huyo hazina ukweli wowote na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.