Zitto akamatwa na polisi Dar

Muktasari:

Leo Oktoba 31, 2018 Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni limemkamata Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Kabwe Zitto na yupo kituo cha polisi Oysterbay

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni leo Jumatano Oktoba 31, 2018 limemkamata kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo wa kipolisi,  Jumanne Murilo amethibitisha kukamatwa kwa mwanasiasa huyo ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini na kwamba anahojiwa katika kituo cha polisi Oysterbay.

“Ni kweli tumemkamata  tunaendelea na mahojiano naye,” amesema Murilo na alipoulizwa sababu za kumkamata amesema, “Taarifa za kina tutatoa baadaye.”

Jana, Jeshi la Polisi mkoani Kigoma lilimtaka Zitto kuwasilisha vielelezo juu ya kauli aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari Jumapili iliyopita Oktoba 28, 2018 kuwa ana taarifa za wananchi zaidi ya 100 kuuawa katika tukio la mapigano ya wananchi wa jamii ya Wanyantuzu na polisi wilaya ya Uvinza mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno amesema tuhuma za mbunge huyo hazina ukweli wowote na kusisitiza kuwa ni upotoshaji unaofanywa na wanasiasa.