Zitto aachiwa kwa dhamana

Muktasari:

Alikamatwa jana usiku kata ya Kikeo, Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.


Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameachiwa kwa dhamana ya maneno ya Sh50 milioni na kudhaminiwa na wakili wake, Lazarus Mvula.

Kiongozi huyo alishikiliwa tangu jana alipokamatwa kwa kufanya mkusanyiko bila kibali. Zitto alikamatwa katika Kata ya Kikeo iliyopo wilayani Mvomero na alitarajiwa kuhojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dakawa lakini akahamishiwa Morogoro Mjini.

Tangu jana saa 4:42 mpaka saa 5:40 usiku, alikuwa akitoa na kuandika maelezo ya kosa analotuhumiwa kutenda akiwa na wakili Mvula.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Februari 23, 2018 na Mvula inaeleza kuwa baada ya Zitto kulala mahabusu kwa sababu za ziara ya kutembelea madiwani wa ACT katika mikoa nane nchi nzima, ameachiwa kwa dhamana.

“Muda huu ameachiwa kwa dhamana ya maneno yenye thamani ya Sh50milioni. Anatakiwa kuripoti Polisi Kituo Kikuu cha Polisi cha Mkoa wa Morogoro Jumatatu, Machi 12, 2018,” inaeleza taarifa hiyo.