Watu 14 wakamatwa kwa kupinga ukomo wa umri kuondolewa

Rais Yoweri Museveni

Muktasari:

  • Gazeti la Daily Monitor limeripoti kwamba polisi waliwakamata vijana hao na kuwatia ndani ya karandinga na kuwapeleka Kituo Kikuu cha Polisi ambako waliwekwa mahabusu.

Kampala, Uganda. Wanaharakati 14 walikamatwa jana mjini hapa wakati wakipiga kampeni kupinga pendekezo la kuondoa ukomo wa umri hatua ambayo itamwezesha Rais Yoweri Museveni kugombea tena katika uchaguzi ujao.

Gazeti la Daily Monitor limeripoti kwamba polisi waliwakamata vijana hao na kuwatia ndani ya karandinga na kuwapeleka Kituo Kikuu cha Polisi ambako waliwekwa mahabusu.

Polisi hawakueleza sababu za kuwakamata wanaharakati hao ambao wote walikuwa wamevaa fulana nyeupe na vipeperushi wakipunga kuashiria kupinga mabadiliko ya katiba. Hata hivyo, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa wanaharakati kukamatwa kwa madai kuwa wamefanya mkusanyiko usio halali.

Julai mwaka huu, kikundi cha vijana wapinzani wa pendekezo hilo walizindua kampeni na walikamatwa kwa kosa la kuandaa mkusanyiko usiohalali.

Mwaka 2005, katiba ilirekebishwa kwa kuondoa ukomo wa mihula miwili uliowekwa ili kumwezesha Museveni kugombea muhula wa tatu. Umri wa miaka 75 ndio ulikuwa kikomo kwa mtu yeyote kugombea urais, na Museveni ambaye ana umri wa miaka 73 sasa atakuwa na umri wa miaka miwili zaidi ikifika wakati wa uchaguzi mwaka 2021.

Septemba 12, kikao cha wabunge wa chama tawala cha NRM na wabunge wa kujitegemea kilipitisha azimio la kuwasilisha muswada bungeni unaopendekeza kufuta Ibara ya 102(b) na kuondoa ukomo wa umri. Muswada huo ulitarajiwa kuwasilishwa bungeni jana.