Sh1.39 trilioni kukuza sekta ya mifugo nchini

Licha ya Tanzania kuwa tajiri wa mifugo barani Afrika, sekta hiyo nchini inachangia asilimia 6.9 tu ya pato la Taifa, wakati viwango vya kimataifa ni kufikia asilimia 30 ya pato hilo.

Tanzania inakisiwa kuwa na asilimia 1.4 ya idadi ya ng’ombe wote duniani na asilimia 11 barani Afrika, ikiwa ya pili kwa kuwa na ng’ombe wengi huku Ethiopia ikiongoza.

Tanzania ina takriban ng’ombe 30.5 milioni, mbuzi 18 milioni, kondoo 5.3 milioni. Mifugo mingine ni pamoja na nguruwe, kuku wa kienyeji na kuku wa kisasa.

Sekta ya mifugo imeajiri asilimia 50 ya wadau ikijumuisha wa moja kwa moja na kwa njia mbadala wanaofikia milioni 4.6.

Hata hivyo, utajiri huo bado haujawakomboa Watanzania wengi hususani wafugaji kwa kukabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uduni wa teknolojia ya kijenetiki, ukosefu wa malisho, magonjwa na ukosefu wa viwanda vya kuongeza thamani.

Wafugaji wenye makundi makubwa ya mifugo wamekuwa wakihamahama ili kutafuta malisho, jambo linalosababisha migogoro ya ardhi sehemu mbalimbali nchini.

Kutokana na ukame na kukosekana maeneo rasmi ya malisho, mifugo imekuwa ikifa kwa kukosa maji na malisho bora.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imekuja na Mpango Kabambe wa Mifugo Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa uchambuzi wa sekta ya mifugo.

Akizundua mpango huo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amekiri kuwapo kwa changamoto zinazokwamisha sekta ya mifugo kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa.

Kuhusu mpango huo, Waziri Mpina anasema Serikali imeshaanza kutekeleza mpango huo kupitia juhudi mbalimbali hasa katika mradi wa uendelezaji zao la maziwa (Paid) unaotekelezwa kwenye mikoa 13. “Kuanzia mwaka 2016 hadi sasa, idadi ya ng’ombe waliohimilishwa katika mikoa hiyo ni 57,162 na idadi ya ng’ombe waliozalishwa ni 33,640,” anasema Mpina.

Mpango wenyewe

Akifafanua kuhusu mpango huo kabambe, ofisa mifugo mkuu, Nathaniel Mbwambo anasema huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo ya awamu ya pili (ASDP II) na utagharimu Sh1.39 trilioni, huku Serikali ikitarajiwa kuwekeza Sh502.6 bilioni (36%) na sekta binafsi Sh891.3 bilioni (64%).

Ili kufikia matokeo chanya katika mifugo, Mbwambo anasema juhudi zinatakiwa kuwekezwa katika uzalishaji wa nyama nyekundu kutoka tani 394,600 mwaka 2016/17 hadi tani 742,500 mwaka 2021/22, japo ongezeko hilo bado halikidhi mahitaji.

“Kuongeza uzalishaji wa nyama ya kuku kutoka tani 63,600 mwaka 2016/2017 hadi tani 465,600 mwaka 2021/22. Ongezeka la nyama ya kuku litasaidia kuondoa upungufu wa nyama nyekundu na kuongeza uzalishaji wa nyama ya nguruwe kutoka tani 22,000 hadi 37,000,” anasema Mbwambo.

Anataja mkakati wa kuendeleza mfumo wa unenepeshaji mifugo na wa ranchi kwa asilimia 100 na 37 kwa mtiririko.

Pia, anataja mpango wa kuendeleza malisho kwa ukubwa wa eneo na ubora kwa kutumia mashamba darasa, huku eneo la viwanda likipewa kipambele kwa kuviongeza viwili.

Kuhusu magonjwa anasema wataongeza chanjo ya mdondo (NCD) kwa kuku wa asili na kupambana na ugonjwa wa African Swine Fever (ASF) unaoathiri nguruwe na kuongeza usafi (Biosecurity), kuimarisha utafiti, mafunzo na ugani.

Maziwa

Katika tasnia ya maziwa, Mbwambo anasema kutakuwa na matumizi ya teknolojia ya uhimilishaji katika makundi ya ng’ombe wa asili na wa ng’ombe wa kisasa.

Anasema mpango ni kuongezeka kwa idadi ya ng’ombe wa maziwa kutoka ng’ombe 782,992 hadi 2,985,000 ifikapo mwaka 2021/22 sawa na asilimia 281 na kuongezeka uzalishaji wa maziwa kutoka lita bilioni 2 hadi lita bilioni 3.8 sawa na ongezeko la asilimia 77.

“Ongezeko la idadi ya ng’ombe wa maziwa litaongeza maziwa na kutosheleza viwanda vya ndani na ziada kwa ajili ya kusindika. Imependekezwa kuwapo na viwanda viwili vya kimiminika na kimoja na unga cha unga,” anasema.

Anashauri kuendeleza unywaji wa maziwa shuleni ili kupanua wigo wa soko.

Zao la ngozi

Kuhusu uzalishaji wa ngozi, Mbwambo anasema kwa mwaka, asilimia 10 ya ng’ombe milioni 28 wanachinjwa na wanatarajia kupata ngozi milioni 2.8 za ng’ombe na ngozi milioni 4.3 za mbuzi na kondoo.

“Kwa sasa kuna viwanda sita vinavyofanya kazi kati ya tisa. Tunatarajia kusindika vipande milioni 1.5 vya ngozi za ng’ombe na 1.8 vya mbuzi na kondoo. Hivyo bado Tanzania ina rasilimali kubwa ya ngozi ambayo haiongezwi thamani,” anasema.

“Mapendekezo ni kuongeza viwanda viwili vikubwa ndani ya miaka mitano pamoja na kufufua vilivyokufa,” anaongeza Mbwambo.

Katika mkutano huo pia walikuwapo mawaziri wa mifugo na kilimo wastaafu.

Waziri wa zamani, Paul Kimiti ameshangazwa na kupungua kwa idadi ya ng’ombe katika ranchi za Taifa.

“Mimi nilikuwa waziri wa mifugo, tulianzisha ranchi za Taifa kwa ajili ya kusaidia wafugaji wadogo wapate mfunzo. Tulikuwa na ng’ombe 80,000, lakini hivi karibuni nimesikia wamefikia 11,000, hao wengine wako wapi? au ndiyo mmewapa wafugaji?”anahoji Kimiti.

Mawaziri wengine wa zamani waliokuwapo ni Dk Charles Tizeba na Titus Kamani.

Akizungumza kwa niaba ya asasi za kiraia, mkurugenzi wa jukwaa la wadau wa kilimo (Ansaf), Audax Rukonge anaishukuru wizara ya mifugo kwa kuanzisha dawati la sekta binafsi akisema litasaidia wadau kufikisha kero zao.

“Sisi kama Ansaf tunazo taasisi 50 za wafugaji tunazosimamia, tunaamini zitafaidika na dawati hili,” anasema Rukonge.