Sheria inatoa haki mbili kwa kazi za sanaa

Umiliki wa mali ni moja kati ya haki muhimu zinazotambulika kisheria hata Katiba ya Tanzania katika inaItambua na kuilinda.

Haki hii imesababisha kutungwa kwa sheria mbalimbali zinazolinda na kutoa utaratibu juu ya mambo yanayohusiana na mali binfsi za watu.

Moja ya mambo ambayo sheria inayalinda na kuyatetea ni haki za ugunduzi na utunzi wa mambo mbalimbali yahusuyo sanaa kwa Sheria ya makimiliki ya haki shiriki ya mwaka 1999.

Sheria hii inatoa miongozo juu ya ulinzi wa kazi mbalimbali za sanaa kama inavyoainishwa katika vifungu mbalimbali vya sheria hiyo. Inatambua na kulinda kazi za sanaa kama muziki, maigizo na zinazofanana na hizo.

Lakini kwa kazi yeyote kuwa na haki ya kulindwa kisheria ni lazima iwe halisi, yaani yeyote anaedai kuwa ni mmiliki awe ni muanzilishi au mtunzi wa kazi hiyo ili kutambua nguvu na maarifa yaliyowekezwa.

Haki za wasanii na kazi za sanaa Tanzania zinalindwa na kuelezewa na sheria. Kazi hizo ni kama muziki, maigizo, hadithi, ngonjera, soga, uandishi wa kazi mbalimbali na mengineyo.

Ulinzi huo wa kazi za sanaa unaenda mbali hata ngazi ya kimataifa kwa sababu kwamba Tanzania ni mshiriki na sehemu ya makubaliano ya kimataifa yanayotoa ulinzi wa kazi hizo.

Ili msanii au mtengenezaji wa kazi ya sanaa apate stahiki za kisheria ni lazima kazi yake iwe imetengenezwa au kuwasilishwa kwani sheria haitoi ulinzi kwa mawazo bali uwasilishaji wa mawazo hayo kupitia sanaa husika.

Sheria inatoa haki za aina mbili kwa kazi za sanaa zilizotengenezwa au kuwasilishwa. Haki hizo ni heshima ya ugunduzi na haki ya kuitumia kazi hiyo kujipatia kipato.

Yeyote anayetumia kazi ya msanii bila ridhaa au ruhusa ya mmiliki atakuwa anakiuka haki hizo na atakua anafanya kosa kisheria na huo ni wizi au uharamia wa kazi za sanaa.

Hii ni kwa sababu mmiliki hutumia muda mwingi, nguvu na akili kuikamilisha. Hivyo basi, yeyote anayetaka kujiingizia kipato, hana budi kupata ridhaa ya mtunzi.

Baraza la Sanaa Tanzania na Chama cha Hakimiliki Tanzania ni vyombo mahususi vinavyoshughulikia ulinzi na utunzaji wa kazi za sanaa.