Tunaweza kupunguza kuuza malighafi nje

Friday June 7 2019

 

By Honest Ngowi

Taarifa za baadhi ya nchi kama vile Zimbabwe, Rwanda na Burundi kuonyesha nia ya kununua mahindi nchini zilizopokelewa mwezi uliopita, zimezua mjadala kwa wadau wa kilimo.

Mjadala uliopo unaelekezwa katika muktadha wa uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi na uuzaji wa malighafi kimahususi.

Biashara ya kimataifa huhusisha uuzaji na ununuaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi. Takwimu zinaonyesha Tanzania huuza zaidi malighafi kuliko bidhaa zilizoongeza thamani kwa kuchakatwa. Malighafi hizi zinajumuisha mazao na madini.

Mara nyingi bidhaa hizi huuzwa katika nchi zililizoendelea zaidi kwa lengo la kuchakatwa na kuongezewa thamani kupata bidhaa iliyokamilika tayari kwa kutumiwa. Takwimu pia zinaonyesha Tanzania hununua zaidi bidhaa kutoka nchi zilizoendelea kama mavazi, mitambo, dawa na kadhalika.

Nchi hufaidi zaidi katika biashara ya kimataifa kama itauza bidhaa na huduma zilizoongezewa thamanni kuliko zisizoongezewa thamani.

Malighafi zote huongezewa thamani kwa kuchakatwa. Uongezaji thamani unakuja na maendeleo na faida nyingi za kiuchumi ambazo ni pamoja na ajira, ongezeko la matumizi ya bidhaa na huduma na kuimarika kwa ubora bidhaa au huduma husika.

Advertisement

Kuongeza thamani ya malighafi ndani ya nchi kunachangia mapato ya Serikali kuu na za mitaa yatokanayo na kodi, tozo na ushuru kutokana na miamala mbalimbali.

Bidhaa inapochakatwa na kuongezewa thamani ndani ya nchi mabaki yake hutumika kama malighafi au bidhaa ya mwisho. Uongezaji thamani ndani ya nchi huleta mwingiliano wa kisekta.

Mahindi

Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya uchumi wa viwanda na uuzaji wa malighafi nje ya nchi. Malighafi za kilimo au madini zinapouzwa nje bila kuongezewa thamani kunapoteza fursa ya kujenga na kuimarisha uchumi.

Kuongeza thamani ndani ya nchi ni fursa kwa viwanda na mnyororo mzima wa thamani na mafundo yake. Katika azma ya Tanzania ya viwanda kuuza malighafi nje ni kutotumia vizuri fursa ya kuwa na viwanda vinavyotumia malighafi zilizopo kutoa ajira.

Mwishoni mwa mwezi uliopita kumekuwa na habari kuhusu soko la mahindi nje ya Tanzania hasa Burundi na Rwanda ambako zinakadiriwa kuhitaji zaidi ya tani 100,000 kila moja na Zimbabwe inayotaka tani 800,000.

Kuuza mahindi katika masoko ya nje kiuchumi ni kupeleka ajira kwa vijana wa huko, kipato na faida nyingine zitokanazo na kuongeza thamani ndani ya nchi kwa wananchi wa huko ambao watakuwa na fursa ya kuchangamkia ucjakataji wake.

Ni kupoteza fursa ya kujenga na kuimarisha uchumi wa viwanda hasa vinavyoongeza thamani mazao ya kilimo na bidhaa zake. Kuuza mahindi badala ya unga na mazao mengine sio afya katika muktadha wa uchumi wa viwanda.

Ushauri

Ili kupunguza uuzaji wa malighafi kama za kilimo na madini nje ya nchi, ni muhimu kuimarisha misingi ya uchumi wa viwanda kupitia kuongeza thamani malighafi hizi.

Kati ya mambo ya kuendelea kufanya ni kuwa na mazingira rafiki, mazuri na ya kuvutia uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani yakiwamo ya kisera, kisheria na kiudhibiti. Pamoja na haya, ni lazima kufanya utafiti wa masoko ya nje ya malighafi ili kujua mahitaji ya mlaji wa mwisho.

Kwenye mahindi kwa mfano, ni muhimu kumfahamu mteja wa Zimbabwe, Rwanda, Burundi na kwingineko na anatumia mahindi yakiwa katika hali gani. Yanaweza kuwa ni mahindi na bidhaa zake kama vile unga na pumba.

Inawezekana, mahindi na bidhaa zake zinatumika kwa ajili ya vyakula vya mifugo, viwandani kama vile kutengeneza mafuta ya binadamu au ya mitambo au pombe.

Tukijua mlaji wa mwisho anataka nini itasaidia kujipanga kuzalisha katika viwanda vya nyumbani na kupata faida zitokanazo na kufanya hivyo ukilinganisha na kuuza malighafi nje.

Advertisement