Umuhimu wa kikosi kazi cha kodi kwa mfumo shirikishi

Serikali zote duniani ikiwamo ya Tanzania huitaji fedha kwa ajili ya kugharamia bidhaa na huduma za umma. Bidhaa na huduma za umma ni zile ambazo hazitolewi na sekta binafsi kwa sababu zilivyo.

Huweza kuwa huduma ambazo kiuchumi hazilipi au zinahitaji uwekezaji mkubwa kuliko ambavyo sekta binafsi inavyoweza kuwa na utayari na uwezo wa kuwekeza.

Bidhaa na huduma hizi ni pamoja na elimu, afya, maji, miundombinu ya kiuchumi kama barabara, bandari, reli na viwanja vya ndege.

Pia, Serikali zina wajibu wa kutoa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao.

Ili kufanya yote haya fedha nyingi zinahitajika. Fedha hizi hutoka katika vyanzo mbalimbali vikiwamo vya kikodi na visivyo vya kikodi.

Kodi ni kati ya vyanzo vikuu endelevu na vya uhakika vya mapato ya Serikali nyingi. Pamoja na mambo mengine, mfumo wa kodi ni lazima uwe shirikishi ili nchi ikusanye kiasi kikubwa cha kodi bila kuathiri walipa kodi.

Umuhimu wa kodi

Nchi inayokusanya kodi ya kutosha huepuka kukopa hivyo kuzuia ongezeko la deni la Taifa na athari zake hasi.

Athari hizi ni pamoja na karaa zitokanazo na deni kama vile masharti magumu na garama za kulipa deni na riba yake.

Kukusanya kodi vizuri hupelekea nchi kuepuka kutegemea misaada ya wafadhili ambayo huweza kuwa na kero kama za masharti magumu, kutotoka kwa wakati na kiasi kilichokubaliwa na kuhitajika.

Kwa upande wa wananchi, ulipaji kodi huifanya Serikali kuwajibika kwao zaidi kuliko kuwajibika kwa wafadhili na wakopeshaji.

Kati ya mbinu za kuwa na makusanyo mazuri ya kodi yasiyoathiri walipaji ni kuwa na mfumo wa kodi ulio shirikishi. Kati ya jitihada zilizofanywa ili kuwa na mfumo shirikishi wa kodi Tanzania ni kuwapo kwa kikosi kazi cha kodi.

Mbinu shirikishi

Tafiti za uchumi na maendeleo zitaonyesha kuwa kuna faida kubwa kutumia mbinu shirikishi katika mambo mbalimbali ya maendeleo kulingana na hali halisi iliyopo. Mbinu shirikishi ni juu ya kupata maoni, mawazo, mitizamo, malalamiko, kero na mambo kama hayo kutoka kwa wadau wa jambo husika.

Wadau hawa ni wale wanaoguswa na jambo husika kwa njia chanya au njia hasi. Wanaweza kuwa wanapinga au wanaunga mkono jambo hilo.

Umuhimu wa kushirikisha

Ni muhimu kupata maoni ya wadau wengi iwezekanavyo kupitia mbinu shirikishi zilizo sahihi. Mbinu shirikishi ni muhimu kwa kuwapo kukubaliana, kuungwa mkono, kuelewana na umiliki wa pamoja wa jambo husika.

Yote haya ni muhimu sana katika kufikia mafanikio ya mipango kadhaa ikiwamo ya uchumi kama vile kufikia malengo ya kikodi. Ni katika muktadha huu kikosi kazi cha kodi Tanzania kinakuwa muhimu katika kuwa na mfumo wa kodi shirikishi na faida zake.

Kikosi kazi cha kodi

Kikosi kazi cha kodi Tanzania kinaratibiwa na Wizara ya Fedha na Mipango na kuundwa na wadau mbalimbali wa kodi.

Wadau wa kodi hupeleka maoni yao kuhusu maboresho ya kodi kwa sekretarieti ya kikosi kazi. Wadau hawa ni pamoja na sekta ya umma, sekta binafsi, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanazuoni, watafiti, wataalamu wa uchi na umma kwa jumla.