Usimuamini mtu kupita kiasi katika mkataba

Angalia uhalali wa mkataba wenyewe;

watu wengi wameingia katika makubaliano ambayo huita ni mikataba lakini ukiichunguza vizuri kisheria, utakuta siyo mikataba bali ni makubaliano tu ya aina fulani, ambayo hayana nguvu yoyote kisheria.

Ili makubaliano yoyote unayoyafanya yawe na nguvu ya kisheria au halali kisheria ni lazima yawe na nia ya kuwajibika kisheria katika malipo halali, uwezo au mamlaka ya kuingia katika mkataba, hiari na uhalali wa jambo lenyewe ambalo watu wenyewe mmekubaliana.

Usiingie katika mkataba wowote kama mambo hayo matano hayapo. Kukosekana kwa jambo mojawapo kati ya hayo kunaondoa uhalali wa mkataba au makubaliano hayo.

Usimuamini mtu kupita kiasi; watu wengi wamekuwa wakifanya makubaliano ya maneno kwa sababu tu mtu ni mzazi wake, ndugu, muumini mwenzake, mchungaji wake, sheikh au imamu wake, mwalimu wake, bosi wake, mfanyakazi mwenzake au rafiki yake na mwisho wakaishia kujuta kwa nini alimwamini mtu huyo kiasi hicho.

Mwenye tatizo hapo hakuwa huyo ndugu. Mwenye tatizo ni wewe ambaye ulimwamini kupita kiasi, wakati hakuna binadamu duniani anayepaswa kuaminiwa kwa kiasi hicho hasa katika mali au fedha. Tatizo lako tu ni kwamba, hukumtengenezea mazingira ya kuwajibika kisheria, ndiyo maana ikawa rahisi kukuliza.

Hakikisha mkataba wenu ni wa maandishi; usiingie kwenye makubaliano ya maneno kwa sababu tu mtu huyo unamfahamu, atakuja kukushangaza atakapokuja kukugeuka, ingawa wewe ulimwamini na hukutaka makubaliano yenu yawe ya maandishi.

Hakikisha kama umeajiriwa, kunakuwa na mkataba wa kazi kati yako na mwajiri wako, kama umemkopesha mtu pesa kuna mkataba kati ya mkopaji na mkopeshaji bila kujali kiwango cha fedha iliyokopeshwa, kama umenunua kitu kuwe na mkataba kati ya muuzaji na mnunuzi au nyaraka (risiti) inayothibitisha ununuzi huo na jambo lingine lolote ambalo utataka kulifanya kama mtu binafsi au taasisi.

Itaendelea

iv. Washirikishe wenzako/mwenzi wako

Jambo la msingi sana unapotaka kuingia mkataba wa taasisi, jumuia, jamii, kanisa, msikiti, kikundi au familia ni muhimu sana kuwashirikisha wahusika wakuu au wadau katika taasisi hiyo ili nao washiriki na kutoa maoni yao kuhusiana na mkataba huo kabla hamjaingia kwenye mkataba.

Usiingie mkataba kwa pupa. Haraka haraka siku zote huwa haina baraka. Hata kama ngoja ngoja huumiza matumbo, ni vyema ukasubiri kidogo kuliko kukosa baraka za wenzako ambazo ni muhimu sana kisheria.

Hata kama wewe ndiye mkurugenzi mkuu, mwalimu mkuu, sheikh, mchungaji au baba wa familia usithubutu kufanya uamuzi unaoathiri mustakabali wa taasisi bila wahusika wakuu kuwa na taarifa.

Kutokana na kuathiriwa na mfumo dume, waume wengi wamefanya uamuzi na kuathiri hatima ya familia zao bila kumshirikisha mke au watoto. Usithubutu kufanya hivyo.

v. Muone mwanasheria

Ni muhimu pia kumuona mwanasheria ili aweze kukusaidia katika kuandaa mkataba na kukushauri namna ambavyo mkataba huo unapaswa uwe kabla hujaingia katika mkataba huo.

Unaweza ukafikiri unaokoa gharama kwa kufanya mikataba kienyeji, lakini hasara utakayoingia hapo baadaye yaweza kuwa ni nyingi zaidi ya ile gharama ambayo ulidhani kuwa umeiokoa.

Hakikisha mkataba wako umesainiwa na kugongwa muhuri na mwanasheria, kwa sababu mwanasheria huyo atafanyika msaada kwako endapo mwenzako atavunja au hataheshimu vipengele vya mkataba huo.

Usisubiri mambo yakuharibikie ndipo uanze kutafuta msaada wa kisheria. Ni vyema ukachukua tahadhari kabla ya hatari. Japokuwa wakati mwingine kinga huwa na gharama, lakini ni bora ukawa na kinga ya kisheria itakayokulinda katika hali zote za mikataba yako, kuliko kusubiri usumbufu utakaoupata wakati unatafuta tiba ya sheria.