ATCL yaipa StandardAero kazi ya matengenezo ya injini za Bombardier

Wednesday November 14 2018

 

By Ephrahim Bahemu, Bahemu [email protected]

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limeingia mkataba na kampuni ya StandardAero itakayokuwa ikizifanyia matengenezo makubwa injini za ndege zao aina ya Bombardier Q400.

Mkataba huo wa makubaliano umesainiwa leo Jumatano Novemba 14 ambapo upande wa ATCL aliyesaini ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara,  Patrick Ndekana huku upande wa StandardAero mtia saini akiwa ni Tayeb Bouhassis ambaye ni mkurugenzi wa mauzo wa kanda.

Ndekana amesema kwamba kampuni hiyo itakuwa ikifanya matengenezo makubwa ambayo hayawezi kufanywa katika karakana za shirika hilo.

"Tunajivunia kufikia mkataba huu hii ni miongoni mwa kampuni za kimataifa iliyopewa idhini na Bombardier kufanya matengenezo katika injini zao, ndege zetu za aina hiyo zinatumia injini aina ya PW150A," amesema Ndekana.

Kwa upande wake Bouhassis amesema wanajivunia kuingia mkataba na kampuni inayokuwa haraka na kujiimarisha vizuri katika ukanda huu.

"Tunafuraha kwa kuwa huu kwetu ni mwanzo mpya wa kufanya kazi na kampuni kama hii ambayo inaendelea kukua, tunatarajia kufanya nao kazi zaidi kwa baadaye," amesema Bouhassis ambaye kwa hapa nchini kampuni yao inahudumia mashirika mengine kama Precision Air, Coastal Aviation na nyinginezo.

Mkuu wa kitengo cha ufundi wa ATCL, Righton Mwakipesile amesema kampuni ya StandardAero imekuwa ikitoa huduma katika shirika hilo tangu mwaka 2015 kwa ndege yao aina ya Q300 hivyo anaifahamu vizuri kwa ufanisi wa kazi na huduma zao.

"Kawaida Q400 inafanyiwa matengezo makubwa ya injini ikisharuka masaa 5,000 matengenezo hayo ambayo ni ya kawaida hata kama ndege haijaonyesha kuwa na hitilafu huchukua siku 21 tu, hawa StandardAero kituo chao kikuu cha matenfenezo kipo nchini Singapore," amesema Makipesile.

Advertisement