Fursa za maonyesho china na malalamiko ya upendeleo

Kwa muda mrefu, uhusiano wa Tanzania na China umekuwa ukilenga kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili. Ukiacha miradi mikubwa ya kiserikali, wajasiriamali pia hupewa fursa.

Miongoni mwa fursa zinazotolewa kutokana na diplomasia ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizi ni maonyesho ya biashara.

Kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma, Tanzania imepewa banda yenye ukubwa wa mita za mraba 50 kushiriki maonyesho ya kimataifa nchini humo yajulikanayo kama International Horticulture Expo 2019 yatakayofanyika jijini Beijing kwa miezi sita mfululizo.

Wiki iliyopita, balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alikutana na Jiao Yutong, mkurugenzi wa sekretariati ya maonyesho hayo yatakayofanyika kuanzia Aprili 29 hadi Oktoba 7, na kutiliana saini ya ushiriki.

“Wafanyabiashara wa Tanzania watapata fursa ya kutangaza bidhaa. Aidha katika kipindi hicho, kutakuwa na siku ya Tanzania na utafanyika mkutano wa kuvutia uwekezaji na kutangaza utalii,” anasema Balozi Kairuki.

Kwa kuwa banda hilo si kubwa lakini muda wa maonyesho ni mrefu, Kairuki anasema wamependekeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania ufanyike kwa awamu ili wengi zaidi wapate wasaa wa kutangaza bidhaa zao katika soko la China

Kuhusu gharama za kushiriki, Kairuki anasema ubalozi umekubaliana na sektetarieti ya maandalizi ya maonyesho hayo kwamba Serikali ya China itafadhili malazi kwa washiriki wa Tanzania.

“Wajasiriamali wanatakiwa kujilipia nauli tu kuja kutafuta wateja China,” anabainisha Kairuki.

Kuanzia wiki iliyopita baada ya Serikali kusaini mkataba huo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) ina jukumu la kutangaza, kupokea na kuratibu maombi kutoka kwa wajasiriamali wakongwe pamoja na wapya waliopo na wenye nia ya kushiriki.

Mkurugenzi mkuu wa TanTrade, Edwin Rutageruka anasema kwa utaratibu walioundaa, kati ya wajasiriamali sita hadi saba watakuwa wanaenda China kuonyesha bidhaa zao kwa wiki mbili na kuwapisha wengine.

Anasema wametangaza taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii pamoja na kupeleka taarifa kwa vyama vya wajasiliamali, kama wanaolima mbogamboga na maua, pamoja na maembe.

Kwa wajasiriamali watakaopenda kuhudhuria maonyesho hayo, Rutageruka anasema wanaweza kuendele akutuma maombi yao mpaka wiki tatu kabla ya kuanza wakati dirisha hilo litakapofungwa.

“Mjasiriamali yeyote mwenye bidhaa inayokidhi vigezo, anaruhusiwa kuomba kushiriki. Akifika hapa tutampa vigezo vinavyokubalika kwenye soko la China. Ni lazima avitimize,” anasema mkurugenzi huyo.

Pamoja na fursa hiyo nyeti inayoweza kuwaongezea soko wajasiriamali nchini, yapo malalamiko kuwa Tantrade ina hodhi taarifa hivyo kuwapeleka wafanyabiashara walewale kila mwaka. Inadaiwa kuwa kitendo hicho hupunguza mchango kwa Watanzania wengi zaidi.

“Tanzania inapewa nafasi kukuza ushawishi wake China, lakini urasimu uliopo TanTrade unasababisha wapeleke wafanyabiashara wachache hivyo kuharibu maana nzima ya mpango huo,” alisema mmoja wa watu wanaolalamikia urasimu huo, ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini.

Kuhusu tuhuma za upendeleo, Rutageruka anasema kuna mfanyabiashara mmoja kutoka Arusha anayesambaza maneno dhidi ya taasisi hiyo.

“Mpaka sasa tumepokea maombi ya wajasiriamali wengi, watakuwepo wale wa kila mwaka na wapya pia. huyo kijana alitaka awe kamishna wa maonyesho haya. Hiyo nafasi ni balozi, hawezi kuwa yeye,” anasema.