Same kituo cha kuuzia vito

Muktasari:

Aliwataka mkuu wa wilaya hiyo, Rosemary Senyamule na mkurugenzi wa halmashauri kusimamia vyema rasilimali hizo ili kukuza uchumi wa wilaya na taifa.

Same.Siku chache baada ya Rais John Magufuli kutoa agizo kwa wakuu wote wa mikoa yote yenye madini kufungua masoko ya kuuzia madini ikiwamo dhahabu, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira juzi amezindua kituo cha kwanza cha kuuzia madini ya vito wilayani Same.

Akizungumza mara baada ya kuzindua kituo hicho juzi, Mghwira alisema wameifanya Same kuwa kituo cha kwanza cha kuuzia madini kutokana na wingi wa madini hayo yanayopatikana wilayani humo.

Alisema lengo la kuanzishwa kituo hicho ni kuzuia utoroshaji wa madini hayo kwani kumekua na tabia ya watu wasio waadilifu kuuza na kufanya biashara ya madini hayo bila kufuata utaratibu na kuwa na leseni.

Aliwataka mkuu wa wilaya hiyo, Rosemary Senyamule na mkurugenzi wa halmashauri kusimamia vyema rasilimali hizo ili kukuza uchumi wa wilaya na taifa.

Naye Senyamule alisema kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na sekta ya madini watahakikisha madini hayo hayauzwi nje ya kituo hicho na watapita maeneo mbalimbali kutoa elimu ili watu wote watumie kituo hicho kuuzia madini.