Wakulima wataka mbegu za asili zisipuuzwe

Muktasari:

Katika Siku ya Chakula Duniani wakulima wametoa changamoto kuwa mbegu za kisasa hazina uwezo wa kupandwa baada ya kuvunwa, hivyo mbegu za asili ziwekewe mkazo

Dodoma. Wakulima wadogo wameiomba Serikali  kuzitambua mbegu asili kwa kuwa zinastahimili ukame na magonjwa tofauti na mbegu za kisasa.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa na wakulima wadogo kutoka mikoa ya Dodoma, Mbeya, Arusha,  Singida, Iringa, Dar es Salaam na Morogoro kwenye maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Action Aid Tanzania jijini hapa.
Mmoja wa wakulima hao kutoka Arusha, Paulina Aloyce amesema mbegu za asili zimekuwa zikitumika tangu zamani na zinatoa mazao ya kutosha tofauti na mbegu za kisasa ambazo wakati mwingine wakipanda hazioti.
"Mbegu zetu za asili ni zile tunazozihifadhi baada ya kuvuna mazao na tunazihifadhi kwa ajili ya kilimo cha msimu unaofuata na hazina madhara yoyote labda tu mvua isinyeshe," amesema Aloyce
 "Lakini mbegu za kisasa hauwezi kurudia kupanda tena (baada ya kuvuna) hivyo unakuwa mtumwa wa kununua mbegu kila msimu na wakati mwingine zinaweza zisiote kabisa."
Ameiomba Serikali kuwasaidia wakulima hao kuwapa teknolojia ya kuhifadhi mbegu za asili ili ziweze kudumu kwa muda mrefu bila kuharibika kwa kuwa hizi za kisasa zinashambuliwa haraka na magonjwa.
Mkurugenzi wa Shirika hilo Bavon Christopher amesema  kilimo hai ndiyo mkombozi wa afya za Watanzania.
Amesema watu wengi wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali hasa yale yasiyo ya kuambukiza kwa sababu ya kutumia mbegu za kisasa zinazohatarisha afya za walaji.
Ameiomba Serikali kuwasaidia wakulima wadogo nchini kupata masoko ya uhakika na kupewa teknolojia za kisasa za kuzalisha kwa tija.