Papa Francis: Ndoa batili, inawezekana, ila…

Papa Francis

Muktasari:

Ni mageuzi yanayoanza Disemba  ambayo yatalibadili  kanisa

Vatican City. Uamuzi uliofanywa na Papa Francis Jumanne  ya wiki hii kuanzisha mchakato wa kurahisisha wanandoa kuachana kwa talaka au ndoa kutenguliwa, umeshangaza wengi.

Kisheria, uamuzi huu utaanza Desemba 8, siku ambayo Kanisa Katoliki linaanza Mwaka wa Huruma.

Uamuzi huo umeonyesha sura ya pili ya kiongozi huyo mkuu wa Kanisa Katoliki duniani lenye waumini bilioni 1.2 na mwanzo wa mageuzi makubwa katika taasisi hiyo.

Kwanza, utashughulikia suala lililozua utata mwingi kwa muda mrefu miongoni mwa waumini wa kanisa hilo, wakiwamo waliotengana na kuoa au kuolewa,  waliojikuta wakikosa sakramenti ya komunio.

Pili, ni utatoa mamlaka kwa majimbo ya kanisa hilo kote duniani kushughulikia suala hilo badala ya mfumo wa sasa wa kupelekwa makao makuu, Vatican.

Tatu, uamuzi huo unamfanya Papa Francis ajitofautishe na watangulizi wake, Yohani Paul II, (marehemu) ambaye kwa sasa ni mtakatifu na Papa Mstaafu Benedict XVI, waliokuwa na msimamo mkali wa kutopenda mabadiliko.

Nne, Papa Francis aliyezaliwa na kukulia mitaa ya Buenos Aires, Argentina,  atakuwa ameguswa na maisha ya kawaida ya watu waliomzunguka.

Historia ya mchakato

Timu ya wataalamu wa sheria za kanisa na tauhidi (theolojia), chini ya Monsinyori  Pio Vito Pinto,  ilieleza Jumanne mbele ya wanahabari mjini Vatican kuwa uamuzi huo ni wa tatu katika mchakato huo katika miaka 2,000 ya kanisa hilo, baada ya marekebisho ya mwisho,  mwaka 1741 na 1908.

Mabadiliko hayo yanaonekana kuwalenga masikini na watu wengine ambao ndoa zao zimevurugika kwa sababu mbalimbali, lakini ambao gharama za kushughulikia marekebisho yake zimekuwa kikwazo.

Vatican,  inaeleza kuwa inafanya marekebisho hayo kuwa rahisi kwa Wakatoliki kubatilisha ndoa zao,  kwa  kuzingatia kanuni na msimamo wa Papa Francis,  ambaye amekuwa nyuma ya mageuzi makubwa ndani ya kanisa hilo, huku akikosolewa na watu wenye msimamo mkali ndani ya kanisa hilo.

Pia, mchakato wa kubatilisha ndoa umekuwa ukikosolewa  kuwa mgumu, wenye gharama na usioweza kufikiwa kirahisi na watu wengi.

Kanuni zilizopitishwa  zitaharakisha mchakato wa kubatilisha ndoa kwa njia rahisi na zinazowezekana, ingawa utaruhusu rufaa kufanyika kirahisi kwa viongozi wa majimbo husika badala ya  Vatican.

Papa Francis anaeleza kuwa mabadiliko hayo hayatashawishi au kupendelea, kuendekeza tabia zinazohalalisha ubatili wa ndoa, badala yake utabadili muda ambao mchakato umekuwa ukitumia.

Kiongozi huyo anaeleza kuwa mchakato huo utakuwa huru na usio na  gharama.

Anaeleza  kuwa mabadiliko ya mchakato huo yamefanyika kwa kuzingatia mioyo ya waumini  wengi ambayo imesubiri ufafanuzi kwa miaka mingi, kiasi cha kujikuta wakiumizwa na kubaki kizani.

Papa Francis na watangulizi wake

Tofauti na watangulizi wake, Papa Yohani Paul II (mtakatifu) na Papa Mstaafu Benedict XVI, kwa upande wao walifikiria kupunguza idadi ya ndoa zinazotenguliwa, wakiamini kuwa mchakato kama huo utaliathiri kanisa.

Wataalam waliosimamia mchakato huo walieleza kanisa kamwe halitaathiriwa na uamuzi huo, badala yake litaendelea kuwa imara kwa kuzingatia kanuni, maadili yake yanayohusu ndoa.

Chini ya utaratibu huo, wanandoa wanaofikiria kutengana hawalazimiki tena kusaka uthibitisho wa pili wa azma yao baada ya suala hilo kushughulikiwa na mahakama ya kanisa kama ilivyokuwa awali.

Kwa kesi ambayo itakuwa ya moja kwa moja, jopo hilo la wataalamu linaeleza kuwa uamuzi wa kubatilisha ndoa utafanywa na askofu wa jimbo.

Katika hilo, Papa Francis  amewashauri maaskofu kuanzisha mfumo utakaosimamia waumini wao waliotengana na wanaofikiria kuvunja ndoa.

Miongoni mwa sababu ambazo pande husika zitazingatia wakati wa kufikiria kubatilisha ndoa ni,  ushahidi kwa mmoja wa wanandoa alikuwa na uhusiano na mwanamke au mwanaume mwingine wakati  akifunga ndoa, mwanamke alitoa mimba au mmoja wao hakuwa wa imani na mwenzake.

Mabadiliko hayo yatasaidia waumini wanaofikiria kuingia katika ndoa mpya, ndoa zao zitambuliwe na kanisa na kwa maana hiyo waruhusiwe kushiriki maisha ya kawaida ya kanisa, zikiwamo sakramenti.

Nchini Marekani, imekuwa rahisi kwa ndoa kubatilishwa, mchakato huo umekuwa  mgumu katika nchi nyingine, zikiwamo Argentina na Chile, zenye  waumini wengi wa Kikatoliki ambazo mchakato umechukua miaka mingi.

Tofauti na mfumo wa kutoa talaka, ambako ndoa inavunjwa,  mfumo wa kubatilisha  ndoa umekuwa mgumu na kuachiwa mamlaka hiyo kwa uongozi wa kanisa baada ya  kujiridhisha kwamba ndoa hiyo ilifungwa bila kuzingatia kanuni.

Sababu kadhaa zikiwa za mmoja au wawili kuingia mkataba huo bila kujua kwamba hicho ni kiapo, bila kutambua kwamba ndoa ilikuwa kifungo cha maisha  au bila kutaka kuzaa watoto.

Tangu achaguliwe kuongoza kanisa mwaka 2013, Papa Francis amekuwa akitaka mchakato huo ubadilishwe na  kulegezwa, jambo ambalo limemfanya aonekane kwa wengi kama mwanamageuzi.

Mara kadhaa, Papa Francis amekuwa akieleza kuwa kubatilishwa kwa ndoa kusichukuliwe kama chanzo cha mapato kwa kanisa.

Msimamo huo unaonekana kama njia nyepesi, rahisi ya kuwarejesha kanisani  waumini ambao walikata tamaa na kuondoka.

Wiki iliyopita, Papa Francis  alitangaza kwamba mapadri wote wa kanisa hilo waruhusiwe kutoa msamaha kwa waumini wao wakiwamo wanawake waliokiri kutoa mimba.

Uamuzi huo umechukuliwa wakati kanisa likianza  Mwaka wa Huruma, unaoanza   Desemba.

Katika hali ya kawaida, msamaha kwa waliotoa mimba, kosa  linalodhaniwa kwa jicho la Kanisa Katoliki kuwa dhambi kubwa, mhusika hutengwa na kanisa, lakini wakisamehewa na mapadri kwa ruhusu ya maaskofu.

Kanuni hiyo ya kubatilisha ndoa imekuwa ikiwaathiri pia watu wengine  wasio waumini  wa Kanisa Katoliki waliotengana na wanaofikiria kuoa au kuolewa  na Mkatoliki.

Hao, wamekuwa wakitakiwa kuwa na hati ya ubatilisho huo kabla ya kufunga ndoa na Mkatoliki kanisani.

Kwa kawaida, Wakatoliki wanaoachana mbele ya vyombo vya kisheria hawatengwi  na kanisa ambalo linatambua mchakato wa talaka, ambao ni pamoja na ulinzi na uangalizi wa watoto.

Hata hivyo, waumini waliotengana kwa talaka hawaruhusiwi kuoa au kuolewa hadi  ndoa zao zibatilishwe .

Kama Mkatoliki ameoa bila ndoa yake kubatilishwa kwanza, haruhusiwi kupokea sakramenti ya komunio.

Mabadiliko hayo ambayo yametiwa saini na Papa Francis na yataanza Desemba 8 mwaka huu, siku ambayo kanisa linaanza Mwaka wa Huruma, ni  hatua mpya kwa kanisa hilo kujirekebisha.

Nchini Tanzania

Tanzania inao waumini wakatoliki, baadhi yao wamekumbwa na tatizo hilo na wanauonaje uamuzi wa Papa Francis?

Mkazi wa Dar es Salaam, John Lipingu anasema ni hatua nzuri kwa kuwa kanisa limeamua kuangalia na kulegeza sheria zilizotumika kwa takriban miaka 2,000.

“Kwa walioishi zamani,  naamini walikuwa na imani kubwa kulika sasa, hivyo sheria hizo kulegezwa itasaidia wanandoa wengi wenye matatizo kupata ufumbuzi,” anasema.

Anaongeza kuwa mabadiliko ya kiimani na kimazingira yanahitajika ndani ya kanisa kwani wapo wanandoa wanaoishi kwa mateso kwa makosa ambayo hawakukusudia,  lakini sheria za ndoa za kanisa zimekuwa na mlolongo mrefu kutoa uamuzi ama wa wanandoa kuishi tena pamoja au kutengana.

Padri Evodius Nachenga wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, anasema kuwa uamuzi huo utarahisisha utendaji kazi wa kanisa kwa kupunguza muda wa mashauri ya ndoa na mlolongo, huku rasilimali mahalia zikitumika.

“Mawasiliano wa wahusika yatakuwa rahisi ili kuweza kupata mwafaka haraka wa matatizo ya ndoa husika kutokana na ukaribu kati ya wanandoa hao  na watakaosikiliza mashauri kutafuta ufumbuzi,” anasema.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini anasema  ni uamuzi mzuri unaoonyesha kwamba kiongozi huyo ana imani na maaskofu .

“Ni jambo zuri kwani sasa siyo lazima suala hilo liamriwe Vatican, itarahisisha utendaji kazi wa kanisa na maaskofu, lakini hauna maana kama majimbo yawe legelege na kucheza na suala hilo, lazima majimbo yawe makini katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya ndoa.

“Baba Mtakatifu (Papa) ameonyesha kuwaamini maaskofu na majimbo. Mungu hakutaka ndoa iwe mwisho wa kila kitu, bali mwendelezo wa maisha ya maelewano katika familia, kanisa na taifa la Mungu,” anaeleza Kilaini.

Mwanzo wa mageuzi makubwa

Kwa mwaka mmoja au zaidi, wachunguzi wa mambo ya kanisa wamekuwa wakisubiri  kutokea kwa mabadiliko hayo.

Hatimaye, yametokea na sheria ya kanisa kuhusu kutenguliwa kwa ndoa imebadilishwa kiasi cha kurahisisha mchakato wa wanandoa kutengua kifungo hicho cha maisha yao ambacho huaminika kuwa kinatoka kwa Mungu.

Mwaka jana, wakati wa sinodi ya maaskofu na Papa Francis, masuala ya talaka na kutenguliwa kwa ndoa yalijadiliwa kwa kina.

Mwezi ujao, maaskofu hao wanarejea Rome kufanya mapitio ya mjadala huo, huku  uamuzi wa sasa ukiashiria kuanza kwa mabadiliko makubwa.

Uamuzi huo wa Jumanne,  kwa macho ya wengine, ni tetemeko la kwanza ndani ya  kanisa hilo, lakini mageuzi zaidi yanafuata.

Padri John Beal, Profesa wa Sheria za Kanisa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Marekani anaueleza uamuzi huo kuwa unatoa angalizo kuhusu kiapo cha ndoa, uhalali wake na  kama kweli kilichukuliwa kwa umakini na wanakanisa kwa miaka mingi.

Tangu mwaka 1750, ndoa yoyote haikutenguliwa kirahisi, ilihitaji uchunguzi na  kujiridhisha na kuridhiwa na mahakama ya kanisa husika na pia makao makuu ya kanisa hilo, Vatican.

Padri Beal anaeleza uamuzi huo kuwa umeondoa ulazima wa suala hilo kusikilizwa kwa mara ya pili.

Majaribio nchini Marekani

Msomi huyo anaeleza kuwa hiyo ni mara ya pili kwa kanisa hilo nchini Marekani  kufanya majaribio hayo, baada ya mara ya kwanza kufanya hivyo kati ya 1970 na 1983.

Anaeleza kuwa maaskofu wa Marekani walihisi kuwa mchakato huo ulichukua muda mrefu kupita kiasi kabla ya ndoa kubatilishwa, wakaomba ruhusa ya kufanya  majaribio. 

Matokeo yalikuwa yenye kutia moyo, uamuzi wa kesi kwenda Vatican unaondolewa ambako asilimia 90 ya kesi hizo yalimalizwa.

Anaeleza kuwa jambo la kushangaza, licha ya mafanikio hayo, kanisa nchini humo likarejea kwenye mfumo wa awali ulioachwa mwaka 1983.

Kwa kawaida, ndoa ambayo hufungwa mbele ya kasisi na mashahidi wawili imekuwa hairuhusiwi kubatilishwa, anaeleza msomi huyo.

Anaeleza kuwa zipo ndoa ambazo zinaweza kutenguliwa, ikiwa zimefungwa  mbele  ya padri,  mashahidi wawili kikanuni, lakini ikathibitika kuwa mwanaume au mwanamke alikuwa na umri mdogo, walikuwa na udugu au zile ambazo zitaonekana kuwa zililazimishwa.

Hili ndilo kundi  litakaloathiriwa na uamuzi huo wa Jumanne, anaeleza padri huyo akiongeza kuwa sababu nyingine ni endapo mmoja wa wanandoa alikuwa na ugonjwa wa akili, hakuwa tayari kwa tendo la ndoa au alishiriki uzinzi.

Takwimu za ndoa batili

Kitakwimu, ndoa  60,000 zimekuwa zikitenguliwa kila mwaka kote duniani, nyingi kati ya hizo zikiwa nchini Marekani, nchi ambayo ina asilimia sita ya Wakatoliki wote, ingawa inachangia asilimia 55 hadi 70  ya matukio ya ndoa zenye matatizo, linaeleza Shirika la Crux.

“Mafundisho ya kanisa yanazungumzia utukufu wa ndoa, kama siyo mafundisho ya Yesu, yanayoeleza ndoa kuwa ni muunganiko wa kudumu, usiogawanyika,” linaeleza.

Marejeo ya talaka kwa jicho la kanisa

Kanisa Katoliki linaamini kuwa Mungu ndiye mwenye mamlaka kwenye ndoa, ambao ni  muunganiko wa kudumu wa watu wawili walioamua kwa hiari kuishi pamoja.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki

Sura 2382-2386, zinazungumzia mambo yanayochangia kwenye talaka na hatimaye kutenguliwa kwa ndoa.

Sura ya 2382- Yesu Kristu anazungumzia umuhimu wa Mungu, muumba aliyeweka ndoa ambayo haigawanyiki, haivunjwi na mwanadamu yeyote hadi kifo.

Sura ya 2383- Wanandoa wanaambiwa  kuwa utengano  wao ni kwa sababu mbalimbali, lakini ndoa yao itadumu daima, huku malezi ya watoto yakizingatiwa, urithi au mgawanyo wa mali  pia ukiangaliwa.

Sura ya 2384- Talaka ni kosa kubwa, ni lililo kinyume cha maadili. Ni uvunjifu wa mkataba  walioingia wanandoa kwa utashi hadi kifo. Uhusiano wowote na mwanaume, mwanamke aliyeachwa ni uzinzi.

Sura ya 2385- Talaka ni kinyume cha maadili, inaleta mparaganyiko katika mfumo,  familia na jamii. Huwaathiri wanandoa  hata watoto. Sura ya 2386- Sakramenti ya ndoa,  inatiwa majaribuni na kutolewa kwa talaka, hasa kwa mwanadoa mmoja aliyekuwa na dhamira ya kuishi na mwenzake, ambayo haikutimia.

Imeandaliwa na Ndyesumbilai Florian na Exuper Kachenje