Iran yagoma kukabidhi kisanduku cheusi cha ndege ya Ukraine

Muktasari:

Mwezi uliopita ndege ya Ukraine ilidunguliwa kwa bahati mbaya nchini Iran na kuua watu wote 176 waliokuwamo.

Tehran, Iran. Serikali ya Iran imekataa kukabidhi kisanduku cheusi cha ndege ya abiria ya Ukraine iliyodunguliwa kwa bahati mbaya nchini Iran.

Ajali hiyo iliyotokea mwezi uliopita ilisababisha vifo vya abiria 176 waliokuwapo katika ndege hiyo.

Hata hivyo, Iran imesema kisanduku hicho kimeharibika vibaya lakini hakitakabidhiwa kwa nchi nyingine licha ya shinikizo la kufanya hivyo.

Kwa upande wake, waziri wa ulinzi wa nchi hiyo, Amir Hatami alisema kwa sasa kiwanda cha jeshi kimeombwa kusaidia kukikarabati kisanduku hicho.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vilimnukuu waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif leo Jumatano Februari 20 akisema kuwa Serikali yake imechua uamuzi huo baada ya kujiridhisha hauna madhara yoyote.

Awali Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau alimshauri waziri huyo kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusiana na tukio hilo.