Mkuu shirika la Boeing atimuliwa

Muktasari:

  • Lengo ni kurejesha imani ya wateja baada ya kuandamwa na ajali za ndege zake za 737-Max

Washington. Kampuni ya Boeing imemfukuza kazi Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Dennis Muilenburg katika hatua ya kurejesha imani ya kampuni hiyo baada ya ajali mbili mbaya zilizohusisha ndege yake ya 737-Max.

Zaidi ya watu 340 walifariki dunia kufuatia ajali hizo, jambo lililochochea shutuma kwamba Boeing iliweka mbele faida zaidi ya usalama.

Familia za waathiriwa zimeafiki hatua ya kujiuzulu kwa Muilenberg. Hata hivyo, wamesema uamuzi wa Boeing kumuondoa na kumpatia nafasi hiyo mjumbe wa zamani wa bodi yake, kunaacha maswali juu ya wajibu wa kuleta mabadiliko.

Boeing ilimtaja David Calhoun, ambaye alihudumu katika bodi ya kampuni hiyo mwaka 2009 na mwenyekiti wake wa sasa kama mtendaji mkuu na rais.

“Huku kujiuzulu kwa Muilenburg ni hatua nzuri, ni wazi kwamba kampuni ya Boeing inahitaji kufanya mabadiliko ya utawala wake wa kampuni,” alisema Paul Njoroge, ambaye alimpoteza mke wake, watoto watatu na mama mkwe wake wakati ndege ya Ethiopian Airlines chapa 302 ilipoanguka mwezi Machi akinukuliwa na BBC.

Calhoun “si mtu sahihi kwa kazi,” aliongeza.

Zipporah Kuria, ambaye baba yake aliuawa katika ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines , alisema Muilenburg angepaswa kuwa ameondolewa kazini zamani lakini uwajibikaji wa ajali unawahusu wengi.

“Ninajihisi ni kama watu wengi zaidi wangepaswa kujiuzulu ikiwemo mtu anayechukua nafasi ya Muilenburg,” alisema Zipporah.

Mabadiliko muhimu

Boeing imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la uchunguzi mkali dhidi ya ndege za 737 Max kufuatia ajali zake zilizotokea katika kipindi cha miezi mitano, ya kwanza ikiwa ni ya Indonesia na baadaye ya Ethiopia.

Safari za ndege za 737 zimepigwa marufuku kusafiri kote duniani tangu Machi, 2019.

Huku kampuni hiyo ikiwa na matumaini ya kurejesha angani ndege zake ambazo ndizo zinazouzwa zaidi duniani kufikia mwishoni mwa mwaka huu, wakaguzi wa viwango vya ndege nchini Marekani wamesema wazi kuwa haitapata kibali cha kurejea angani haraka

Calhoun, mkurugenzi mtendaji wa masuala ya usalama, atachukua wadhifa wake kuanzia Januari 13.

Lawrence Kellner, mjumbe wa bodi tangu 2011, atakuwa mwenyekiti ambaye si mtendaji mara moja.

“Chini ya uongozi mpya, Boeing itafanya kazi kwa uwajibikaji wenye uwazi kamili, ikiwemo mawasiliano thabiti na Shirikisho la utawala wa safari za anga (FAA), waangalizi wengine wa dunia na wateja wake,” ilisema.

Licha ya kufanya mabadiliko, wakosoaji wakuu wa kampuni hiyo mjini Washington walisema bado wana maswali juu ya mabadiliko ya uwajibikaji ndani ya kampuni hiyo.

Seneta Richard Bumenthal alisema, “Kampuni inahitaji utawala mpya katika bodi na waweke watu watakaochukulia usalama kwa umakini.”

Michael Stumo, ambaye alimpoteza binti yake Samya Rose katika ndege ya Ethiopian Airlines na ambaye amezikusanya familia dhidi ya Boeing, alisema kujiuzulu ni “hatua ya kwanza nzuri kuelekea kuifanya Boeing kuwa kampuni ambayo inatoa kipaumbele kwa usalama na uvumbuzi,”alisema.