Rais Kenyatta aeleza ukali wa Rais Moi

Nakuru, Kenya. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema alishawahi kukumbana na ukali wa Daniel arap Moi.

Daniel arap Moi ni Rais wa pili wa Kenya aliyefariki dunia Jumanne iliyopita baada ya kuungua kwa muda mrefu Kenyatta.

Akizungumza leo Jumatano Februari 12 wakati wa ibada ya mazishi ya kiongozi huyo anayetarajiwa kuzikwa kijijini kwake Kabarak, Nakuru Rais Kenyatta alisema mzee alikuwa zaidi ya mwalimu kwake.

Akieleza namna mkasa uliompata hadi kutambua ukali wa rais huyo wa zamani, Kenyatta alisema kuna jambo alilokuwa amelifanya likasababisha kupigiwa simu na mzee Moi siku inayofuata alfajiri.

Alisema kwa kuwa alikuwa anajua alichokifanya, alishindwa kupokea simu na kumuagiza mkewe apokee na aseme kuwa yeye yuko mbali na simu.

“Nimewahi kupata ukali wa mzee, sisi ndio tunajua kelele ya mzee Moi ni nini, tunaielewa. Kuna siku moja alipiga simu asubuhi saa 11.00 na mimi nilikuwa najua kuna kitu nilikuwa nimefanya; nikajua hii simu iko na tabu,” alisisitiza Kenyatta bila kueleza jambo gani alilokuwa amelifanya na kusababisha apigiwe simu

“Nikamwambia mama (mkewe) we chukua hiyo najua wewe utakuwa sawa, akamuuliza yuko wapi akasema hayuko karibu” alieleza Kenyatta huku mke wake akiwa anacheka

Kenyatta alisema baada ya muda mfupi mzee Moi alirudia ten kupiga simu na mke wake akakataa kuipokea na kumlazimu kupokea mwenyewe.

“Baada ya dakika nyingine tano simu ikalia tena mama akaniambia hii mimi sichukui. Nikasema wacha nichukue, akaniulizia ulikuwa wapi, nikamwambia nilikuwa naoga. Acha moto uwake, wacha moto uwake, simu ikapigwa chini paaaa nikawachwa nimeshikilia simu hivi.

“Ikapigwa tena mara ya tatu baada ya dakika 10 nikawa nasema mzee samahani, samahani akaniambia nataka ndani ya saa moja uwe umefika hapa Nakuru,” alieleza Rais Kenyatta bila kusema kuwa kipindi hicho alikuwa na wadhifa gani.

Hata hivyo, Kenyatta alisema hakuenda Nakuru mpaka wiki moja ikapita kwa kuwa ilishajua kuwa mzee huyo ambaye anazikwa leo alikuwa amekasirika sana.

“Nikaweka simu chini, mimi nikapotea karibu wiki moja nikasema siendi hadi hili joto hii iishe.

Kenyatta alisema pamoja na ukali wa Moi lakini mzee huyo alkikuwa mtu wa kusamehe.

“Lakini vile alikuwa mkali, hivyo hivyo tu akikusamehe amekusamehe na anasahau hayo mambo ya jana yanapita,” alisema.