Umoja wa Mataifa waonya mabadiliko ya tabia nchi kuangamiza dunia

Monday December 2 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres  

Madrid, Hispania. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema joto kali linaloendelea duniani huenda likashindwa kudhibitiwa ikiwa hatua za haraka hazitochukuliwa kukabili mabadiliko ya tabia nchi.

Guterres alisema hayo Jumapili iliyopita Desemba Mosi kuwa kwa sasa hali ya joto duniani inatisha lakini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa na viongozi kwa kuwa hawana utashi wa kisiasa.

Katibu mkuu huyo alisema juhudi za dunia kuzuia mabadiliko ya tabia nchi hazitoshi kufikia malengo.

“Kuna hatari kubwa joto duniani huenda likawa kali kuliko ilivyowahi kutokea kiwango mbacho hakiwezi kudhibitiwa kabisa,” alisisitiza.

Kauli ya katibu mkuu Guterres imekuja siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa wiki mbili wa  mazingira unaotarajiwa kufanyika mjini Madrid, Hispania.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aliongeza kuwa athari za kupanda kwa viwango vya joto ikiwamo hali mbaya ya hewa tayari imeanza kushuhudiwa duniani kote.

Advertisement

Gutteres alisema ili kukabiliana na athari hizo kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kuwa na ufahamu wa kisayansi na njia za kiteknolojia za kudhibiti viwango vya joto duniani.

Katika hatua nyingine, wajumbe kutoka nchi 200 wanatajariwa kupitia na kukamilisha sheria zinazosimamia mkataba wa Paris uliofikiwa mwaka 2015.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili  jinsi ya kuanzisha mifumo ya kibiashara ya kimataifa inayofanya kazi ya kudhibiti viwango vya utoaji gesi zinazochafua mazingira, kuzilipa fidia nchi masikini kwa hasara ilizoingia kutokana na kupanda kwa viwango vya kina cha maji ya baharini na athari nyinginezo za mabadiliko ya tabia nchi.

Advertisement