Huyu ndiye mbunge aliyepeleka nzige bungeni

Muktasari:

Mbunge mmoja nchini Uganda amepeleka wadudu aina ya nzige katika kikao cha Bunge ili kushinikiza Serikali ichukue hatua ya kuwadhibiti.

Kampala, Uganda. Mbunge wa Kaunti ya Ngora Mashariki nchini Uganda, David Obala amepeleka nzige bungeni kama njia ya kuishinikiza serikali ichukue hatua kuwadhibiti wadudu hao.

Video ya mbunge huyo iliyomuonyesha akiwa ameweka wadudu hao katika chupa na kuwawasilisha mbele ya Bunge imesambaa katika mitandao ya kijamii na kusababisha mjadala.

Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Monitor la Uganda, mbunge huyo alisema lengo la kupeleka wadudu hao katika kikao hicho ni kupinga hatua ya serikali ya kuchelewa kushughulikia tatizo hilo.

Mbunge huyo alisema wadudu hao wameharibu kwa kiasi kikubwa mazao katika eneo la Afrika Mashariki na kusababisha upungufu wa chakula.

Hata hivyo, hatua hiyo ilipingwa na baadhi ya wabunge waliomtaka kuondoa wadudu hao ndani ya vikao hivyo.

Baadaye Obala alilazimika kukabidhi chupa hiyo iliyokuwa imejaa wadudu hao kwa afisa wa Bunge mwenye jukumu la kuweka amani ndani ya muhimili huo.

Kufatia hali hiyo, Spika wa Bunge wa Uganda, Rebecca Kadaga alitoa maagizo kwa wizara kilimo kutoa maelezo kila wiki kuhusu jitihada zinazofanywa na serikali ili kudhibiti wadudu hao.

Mpaka kufikia jana wadudu hao wamesambaa katika wilaya 17 nchini Uganda ikiwamo Acholi, Karamoja, Teso na maeneo yaliopo Magharibi mwa mto Nile.

Nyingine ni Abim, Kaabong, Nakapiripirit, Amudat, Agago, Katakwi, Nabilatuk, Moroto, Kitgun, Soroti na Kole.