China yaweka zuio la kuingia nchini humo

Dar es Salaam. China imetangaza kuzuia wageni wote kuingia nchini humo hata kama wana viza au vibali, lengo likiwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
China pia imeagiza ndege za nchi hiyo na zile za kigeni kufanya safari moja tu kwa wiki na hazitakiwi kujaza watu kwa zaidi ya asilimia 75.
Taarifa kutoka China zimeeleza kuwa kulikuwa na wagonjwa 55 nchini humo siku ya Alhamisi, kati yao 54 walikuwa ni wa kutoka nje ya nchi hiyo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema kuwa inasitisha kwa muda watu kutoka mataifa mengine kuingia nchini humo kutokana na kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 duniani.
Zuio hilo linawahusu watu wenye viza na wale wenye vibali vya ukazi, lakini halitawahusu wanadiplomasia na wale wenye viza ya C, ambayo mara nyingi hutolewa kwa wahudumu wa ndege.
Vilevile, watu wanaofanya kazi zinazohusu mahitaji ya kijamii pia wanaruhusiwa kuomba ruhusa hiyo maalum.
Licha ya kuwa virusi vya corona, vilianzia China kwa sasa kuna idadi ndogo sana ya maambukizi ikilinganishwa na Marekani na idadi ndogo ya vifo ikilinganishwa na Italia na Hispania.
Hadi leo Alhamisi Machi 27, 2020 idadi ya walioambukizwa virusi hivyo vya ugonjwa wa corona kwa China imefikia 81, 340 na vifo 3,292.
Kati ya idadi hiyo ya maambukizi, jumla ya watu 565 ni kutoka nje ya China, ambapo imeelezwa baadhi yao ni raia wa kigeni walioingia nchini humo au Wachina waliokuwa wakirudi nyumbani kutoka mataifa mengine.
Katika Jimbo la Hubei ambapo ugonjwa wa corona ndipo ulianzia, hadi siku ya Alhamisi hakukuwa na mgonjwa mpya aliyeripotiwa kupata maambukizi ya ugonjwa huo.
Mji wa Wuhan ambao pia ulifungwa tangu Januari na watu kutakiwa kutotoka nje ya nyumba zao, unatarajiwa kufunguliwa Aprili 8, 2020