Corona yaingia New Zealand, vifo duniani vyafika watu 2,800

Wellington. Mgonjwa wa kwanza mwenye maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19) amegundulika nchini New Zealand.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Februari 28, 2020 na waziri mkuu wa nchi hiyo, Jacinda Ardern imethibitisha kuwa nchi yake imekuwa na mgonjwa mmoja mwenye maambukizi ya virusi hiyo.

Amesema kuwa mgonjwa huyo aliyegundulika kuwa na maambukizi ya corona alirejea nchini humo hivi karibuni kutoka nchini Iran.

Mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 60 amegungulika kuwa na maambukizi ya corona baada ya kupata vipimo na anatibiwa katika hospitali mjini Auckland.

Nchi nyingine zilizoripotiwa kuwa na maambukizi ya corona hivi karibuni ni pamoja na Italia, Iran na Korea Kusini

Ugonjwa huo wa corona ambao umekuwa tishio ulianza nchini China mwaka jana mwezi Desemba na mpaka sasa ugonjwa huo umeenea kwenye zaidi ya nchi 40.

 

Mpaka sasa ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu 2,857 duniani huku kikiwa na maabukizi zaidi ya watu 83,000.