DRC na Uganda kushirikiana katika amani, maendeleo

Muktasari:

Viongozi wa Mataifa ya DRC na Uganda wamekubaliana kushirikiana katika kurejesha amani Mashariki mwa DRC na kupambana na vikundi vya waasi. Pia, watashirikiana katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo huduma za jamii kama vile afya.

Kampala. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya afya, amani na usalama, nishani ,biashara na uwekezaji pamoja na masuala mengine ya maendeleo.

Rais Tshisekedi amekuwa katika ziara ya siku mbili nchini Uganda kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa kibiashara wa mwaka 2019 nchini humo.

Katika suala la usalama na amani ambayo ni changamoto kubwa kwa mataifa hayo mawili, viongozi hao wameazimia kutafuta suluhu ya kuyaangamiza makundi ya wapiganaji na waasi mashariki mwa Congo.

Viongozi hao wametoa mwito kwa wenzao katika kanda ya maziwa makuu kuunga mkono juhudi zao. Pia, marais hao wanaamini kuwa hiyo ndiyo itakuwa hatua ya awali katika kuleta maendeleo ya viwanda, biashara na uwekezaji katika eneo hilo.

Baada ya kukutana kwa siku nne, ujumbe wa DRC uliojumuisha maofisa wa ngazi za juu pamoja na wawakilishi 110 wa wafanyabiashara, waliorodhesha na wenzao wa Uganda masuala ambayo waliyataka viongozi wayazingatia ili kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), masuala mawili yaliyosisitizwa katika mkutano huo ni usalama na ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Walipopokea masuala hayo, marais Museveni na Tshishekedi waliahidi kuanzisha operesheni kabambe kuangamiza makundi ya wapiganaji Mashariki mwa Congo.

Kadhalika Rais wa Congo amefichua azimio lake la kuligeuza eneo la mashariki mwa nchi yake kuwa kitovu cha viwanda.

Amebaini maeneo sita ambayo yanalengwa ili kulifanikisha hilo na pia katika biashara na uwekezaji sambamba na kujenga barabara za moja kwa moja kutoka Uganda badala ya kutegemea tu zile zinazopitia Rwanda.

Kulingana na takwimu za serikali, Uganda iliuza bidhaa za thamani ya Dola za Marekani 538 milioni kwa nchi ya Congo huku nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini na mbao iliuzia Uganda Dola 117 milioni.

Baadhi ya wafanyabiashara wametaja ushuru, michakato ya uhamiaji ikiwemo ada za Viza za usafiri na pia barabara kuwa changamoto zinazostahili kupewa kipaumbele ili kuboresha biashara kati ya Uganda na DRC.

Biashara ambazo zinatarajiwa kufanywa na mataifa hayo mawili zinakadiriwa kuwa milioni 532 kwa mujibu wa ofisi ya taifa ya takwimu Uganda.

Waziri wa mambo ya nje wa Uganda anasema kuwa ushirikiano huo ni mzuri kwa kuwa unazipa nchi hizo mbili wigo mkubwa wa kukua kimaendeleo na kufanya kazi pamoja.

Amani mashariki ya DRC

Ingawa maeneo karibu yote ya DRC yamekuwa yakikumbwa na changamoto za usalama kama vita ama kushambuliwa na waasi mara kwa mara, eneo la mashariki ya nchi hiyo ndiyo lililoathirika zaidi.

Akiongea na BBC siku chache kabla ya kuondoka madarakani mwishoni mwa maka 2018, Rais mstaafu wa nchi hiyo, Joseph Kabila alisema katika mambo ambayo angekuwa na muda zaidi kuyashughulikia ni kurudisha amani kwa taifa hilo.

Mashariki mwa DRC kuna makundi ya kijeshi ya waasi na kikabila mengi kupindukia.

Baadhi ya makundi yanaundwa na raia wa nchi hiyo, lakini kuna makundi mengine makubwa ambayo yanafadhiliwa ama kupambana za serikali za nchi jirani.