Familia ya Malkia Elizabeth wa Uingereza inayopitia kwenye msukosuko baada ya mjukuu wake kujitoa kwenye ufalme

Wednesday January 15 2020

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Malkia Elizabeth II ambaye alizaliwa Aprili 21, 1926 anatajwa kuwa mtawala aliyetawala kwa muda mrefu tangu alipochukua nafasi hiyo Februari 9, 1952 kutoka kwa baba yake Mfalme George VI.

Malkia Elizabeth II ndiye kiongozi wa pili kwa umri mkubwa katika viongozi ambao wapo madarakani hivi sasa akiwa na miaka 93 baada ya Waziri Mkuu wa Malaysia, Mahathir Mohamed mwenye miaka 94.

Mfalme George VI alizaliwa mwaka 1895 na alifariki dunia 1952 na alimwachia kiti hicho mwanaye Malkia Elizabeth II ambaye aliyeolewa mwaka 1947 mwanamfalme Philip ambapo walipata watoto wawili kabla ya kuwa malkia na wengine wawili baada ya kuwa malkia 1952.

Kati ya watoto wanne aliowazaa mmoja wao ni mwanamfalme Charles ambaye pamoja na mke wake Diana Spencer walipata watoto wawili mwanamfalme William aliyezaliwa mwaka 1982 na Harry aliyezaliwa mwaka 1984 kabla ya kutalikiana naye 1996 na mwaka 2005 alimuoa Camilla Bowles.

Uingereza inaundwa na mataifa ya England, Scotland, Wales na Island ya Kaskazini. Taifa hilo ni la ufalme wa kikatiba linalofuata mfumo wa utawala wa bunge.

Advertisement

Katika kurithi nafasi ya Malkia Elizabeth  II hadi sasa kuna orodha ya watu saba wanaotarajiwa ambao ni mwanamfalme Charles akifuatiwa na mwanaye mwanamfalme William na watoto wake watatu ambao ni mwanamfalme, George, bintimfalme, Charlotte na mwanamfalme Louis.

Baada ya hao anayefuatia katika orodha ni mwanamfalme Harry ambaye amegonga vichwa mbalimbali kwa kujiondoa kwenye kazi za kifalme.

Mwanamfalme Harry sio jina geni kwa sababu ya yale yanayoendelea kwenye kasri la Buckingham tangu alipofunga ndoa na mke wake Meghan mwaka 2018.

Harry ambaye amehudumu nafasi mbalimbali Uingereza ikiwemo jeshini na kushiriki vita mara mbili nchini Afghanistan na kuwa mwanamfalme wa kwanza katika familia ya utajiri kwenda vitani ardhini baada ya mjomba wake mwanamfalme Andrew aliyetumiwa helikopta kwenye vita ya Falklands.

Wachambuzi wanadai kuwa mwanamfalme Harry kutokana na kutoona uelekeo wa kuchukua nafasi ya ufalme alifikia maamuzi ya kuachana na familia ya kifalme na kubaki kama watu wa kawaida ila wakiendelea kutoa mchango wao kwa familia hiyo.

Kufuatia hatua hiyo, familia ya kifalme imeeleza kusikitishwa na maamuzi, ikisema ni kama ndoto huku ikihoji itakuwaje kuhusu suala la ulinzi wao.

Wanandoa hao wamesema sasa wanapanga kutumia muda wao mwingi Amerika ya Kaskazini na kujitegemea kifedha.

Taarifa ya Jumba la Kifalme Buckingham, imeeleza kuwa Harry na Meghan wataendelea kumuunga mkono kikamilifu Malkia Elizabeth II.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya makao makuu ya Malkia mazungumzo yanaendelea kati ya Prince Harry na mkewe kuhusu mipango hiyo.

Familia ya kifalme imesema inaelewa kuhusu nia yao, lakini masuala hayo kwa sasa ni magumu na itachukua muda kuyafanyia kazi.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilibainisha kuwa si Malkia wala mwanamfalme William au waandamizi wengine katika falme walijulishwa kuhusu hatua hiyo na kwamba uongozi wa juu wa ufalme umepata pigo.

Kasri ya kifalme limesema suala hilo imelipokea kwa mshtuko mkubwa.

Katika maelezo yao, Harry na Meghan walisema walifikiria uamuzi huo kwa muda mrefu na kufanya maamuzi hayo miezi mingi iliyopita.

Wanandoa hao wamepanga kugawa muda wao kwa nusu kuishi Marekani na nusu Uingereza, kuendelea kumtumikia Malkia na kujihusisha na shughuli za kifalme.

Msemaji wa zamani wa Malkia aitwaye Dickie Arbiter alisema kuwa hafahamu ni namna gani wataweza kugeuza mipango yao.

"Hii ni kama ndoto. Kuna suala la usalama, nani atatoa ulinzi kwao?

"Je, ni nchi gani itawapa ulinzi wa kifalme? Je, ni Canada au? Na nani atagharamia?"

Oktoba mwaka jana Harry na mkewe walilalamika kuingiliwa maisha yao kwa kufuatwa na vyombo vya habari kwa kivuli cha kutoka katika familia ya kifalme.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Harry na mkewe wametoa utetezi wao kuhusu tangazo lao kwamba, wameifikia hatua hiyo baada ya kuwa na majadiliano ya ndani ya nyumba yao wao wawili kwa miezi kadhaa.

Hata hivyo, maamuzi yao yamepingwa kwa kudaiwa kuwa walistahili kupewa idhini ya jambo hilo na kutoa taarifa kabla.

Malengo yao mengine ya kujiondoa katika shughuli za moja kwa moja za kifalme ni kutaka kufanya kazi za kawaida katika kuendesha maisha yao ya kila siku badala ya kutegemea mapato yatokanayo na nafasi zao za kifalme.

Advertisement