Guinea wapiga kura, waandamana na kuibua tishio maambukizi ya corona

Sunday March 22 2020

 

Conakry. Wananchi wa Guinea leo Jumapili Machi 22, 2020 wanapiga kura kuchagua wabunge na kupiga kura ya maoni ya mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo wakati kukiwa na maandamano mitaani yanayotishia maambukizi ya virusi vya corona.

Wapinzani wamefanya mgomo wa kutaka kucheleweshwa kwa uchaguzi huo ambao awali ulipangwa kufanyika Machi Mosi, 2020 wakimtuhumu Rais wa Guinea, Alpha Conde kupanga kutumia mabadiliko ya katiba ili aendelee kubaki madarakani.

Conde ameliongoza Taifa hilo la Afrika Magharibi tangu mwaka 2010, kipindi chake cha pili cha miaka mitano kitakwisha Desemba 2020.

Kwa katiba ya sasa ya Guinea, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 haruhusiwi kuwania muhula wa tatu.

Viongozi wa upinzani wamesema Conde ambaye ndiyo kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, anapanga kutumia mabadiliko mapya kama zana ya kujiongezea muda wa kukaa madarakani.

“Conde anajaribu kubadilisha katiba ili aendelee kukaa madarakani maisha yake yoye,” amesema kiongozi wa upinzani wa chama cha UFDG, Cellou Dalein Diallo kama alivyonukuliwa na Al Jazeera.

Advertisement

“Watu wetu wengi wameuawa wakiandamana kupinga uamuzi huo. Ni haki yao ya kikatiba kuandamana kupinga uamuzi huu,” amesema Diallo ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani.

Mabadiliko ya katiba yanayopendekezwa, hayataji moja kwa moja kwamba Conde ataruhusiwa kugombea katika uchaguzi wa 2020.

Hata hivyo, Rais Conde amekataa kutangaza kwamba hatagombea tena.

“Huo ni uamuzi wa chama. Kwa sasa siyo suala langu,” Conde alinukuliwa na kituo cha Radio France International.

Ili mabadiliko ya katiba yaweze kuridhiwa, zaidi ya asilimia 50 ya kura zitakazopigwa lazima ziridhie jambo hilo.

Kura zinapigwa wakati nchi mbalimbali katika ukanda na bara kwa ujumla zikiwa zimepiga marufuku mikusanyiko ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

 

Tayari watu wawili wamethibitishwa kuwa na maambukizi hayo nchini Guinea.

Tangu Oktoba, wafuasi wa upinzani wamekuwa wakiandamana mitaani wakishinikiza Conde aondoke madarakani baada ya muhula wake kwisha mwishoni mwa 2020. Zaidi ya watu 30 wameuawa katika maandamano hayo wakikabiliana na vyombo vya usalama.

“Tunaandamana kwa sababu Conde ameamua kufanya mapinduzi dhidi ya katiba ya Guinea,” mwanaharakati, Abdoulai Oumou Sow ambaye pia ameshiriki kuandaa maandamano mitaaani, aliliambia Al Jazeera.

Advertisement