Iran kimenuka; waandamaji, polisi wapambana kupinga ongezeko petrol

Muktasari:

Ni raia wa Iran ambao 40 kati yao wakamatwa kwa kosa la kuandamana  kushinikiza kushushwa kwa bei ya mafuta ya petrol.

Iran. Watu 40 wamekamatwa katika mji wa Yazd nchini Iran, baada ya kupambana na polisi wakati wa maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya petroli.

Taarifa ya shirika la habari nchini humo la ISNA ilisema kuwa tukio hilo lilitokea leo Jumapili mchana Novemba 16.

Shirika hilo lilimnukuu mwendesha mashitaka wa Serikali, Mohammad Hadadzadeh akiwwatuhumu waandamanaji hao kusababisha vurugu na uharibifu wa mali.

“Wengi wa waandamanaji si wakazi wa eneo hili wamekuja kuharibu mali na kuondoka,” alisisitiza kiongozi huyo akiongea na kituo hicho cha ISNA.

Hata hivyo, kiongozi hiyo hakuweka wazi ni wakati gani watu hao walikamatwa.

Iran ilikabiliwa na maandamano makubwa siku ya Ijumaa saa kadhaa baada ya tangazo la bei ya petroli kupandishwa kwa asilimia 50 katika lita 60 za mwanzo na asilimia 300 kwa kiasi chochote kitakachozidi kila mwezi.

Katika hatua nyingine, waandamanaji nchini Iraq wafunga barabara.

Waandamanaji hao wanaoipinga Serikali nchini Iraq wamefunga baadhi ya barabara, katika kutekeleza mwito wa mgomo uliotolewa na kiongozi wa kidini mwenye ushawishi mkubwa kutoka madhehebu ya Shia, Muqtada al-Sadr.Waandamanaji hao pia wamejaribu kutawanyika kwenye mji mkuu wa Iraq, baada ya kulidhibiti eneo la kimkakati.