Jinsi mfungwa alivyoiba bilioni mbili gerezani

Abuja, Nigeria. Tumaini Olusegun Aroke, mfungwa anayetumikia kifungo cha miaka 24 jela amepatikana na hatia ya uhalifu wa kimtandao na kuiba Dola za Marekani milioni moja karibu Sh2.3 bilioni.

Mwaka 2012 mfungwa huyo alikamatwa na kuhukumiwa jela miaka 24 baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kimtandao.

Tume ya Kupambana na ufisadi nchini Nigeria, ilisema Aroke alitumia mtandao wa internet kufanya udanganyifu na utapeli ili kujipatia kiasi hicho cha fedha.

Aroke ambaye alikuwa amefungwa katika Gereza la Usalama la Kirikiri, Nigeria uchunguzi wa awali uligundua bado alikuwa akijihusisha na vitendo vya kihalifu akiwa jela.

Taarifa ya Kamisheni ya uhalifu na uchumi (EFCC) ilisema imepokea tuhuma hizo za Aroke ingawa mpaka sasa bado haijategua kindendawili cha jinsi gani mharifu huyo alivyoweza kuendelea kufanya biashara yake ya kinyama kutoka ndani ya gereza.

EFCC ilisema kuwa Aroke ambaye wakati alipokamatwa alikuwa mwanafunzi nchini Malaysia anadaiwa kuwa kinara katika wizi wa kimtandao.

Hata hivyo, uchunguzi wa awali wa EFCC ulibaini Aroke alikuwa akipewa mtandao wa internet kupitia simu yake ya kiganjani na maafisa wa gereza hilo.

“Alikuwa akiwapatia rushwa askari wa gereza na kumruhusu kutumia simu ilikuwa na mtandao wa internet.

“Alikuwa pia amelazwa katika Hospitali ya Polisi ya Nigeria iliyopo mjini Lagos kwa maradhi yasiyofahamika na kuna wakati aliweza kuondoka katika kituo hicho na kukaa katika hoteli, kukutana na mkewe na watoto lakini pia kushiriki shughuli za kijamii zikiwamo harusi na misiba,” ilisisitiza EFCC.

Taarifa ya EFCC pia ilibaini mfungwa huyo alikuwa ametumia jina la uwongo la Akinwunmi Sorinmade kufungua akaunti mbili za benki na kununua gari la kifahari pamoja na nyumba akiwa gerezani.

“Alikuwa na hati ya akaunti ya benki ya mke wake gerezani ambayo alitumia kuhamisha fedha kwa hiari.”

Inaelezwa kuwa kwa sasa maafisa wa kupambana na ufisadi nchini humo wanachunguza ni kwa nini alilazwa hospitalini na ni vipi aliweza kusafiri kwenda kwenye hoteli na maeneo mengine.

Mpaka sasa uongozi wa gereza hilo haujazungumzia tuhuma hizo.

Kesi hiyo imezua gumzo kubwa nchini humo huku wananchi wakihoji ni jinsi gani mfungwa huyo aliweza kutapeli kiasi hicho kikubwa cha fedha akiwa gerezani ikiwamo kutoka na kuhudhuria shughuli za kijamii bila kutambulika na kufanya kazi zake kwa uhuru.