Kifo cha msanii wa Injili chaibua gumzo, Human Rights Watch yataka uchunguzi ufanyike

Muktasari:

Siku moja baada ya kutokea kifo cha msanii wa Injili nchini Rwanda,Kizito Mihigo, akiwa kituo cha Polisi, Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch linataka uchunguzi ufanywe kubaini chanzo cha kifo.

Rwanda. Shirika la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch linataka uchunguzi ufanywe kubaini chanzo cha kifo cha mwanamuziki maarufu wa nyimbo za injili nchini Rwanda, Kizito Mihigo.

Mihigo enzi za uhai wake aliyewahi kutesa na wimbo wa 'Inuma' unaomaanisha njiwa na 'Igisobanuri cy'urupfu' ambao unaelezea kifo ni nini.

Msanii huyo ambaye pia ni mwanaharakati nchini humo, alifariki jana Februari 17,2020 katika kituo cha Polisi Remera, alikokuwa akishikiliwa kwa siku tatu kwa tuhuma za kuruka mpaka wa Kigali kwenda nchini Burundi kwa njia haramu.

Hata hivyo jana alikutwa amefariki kwa kile ilichodaiwa na Jeshi la Polisi nchini humo, kuwa alijinyonga kwa kutumia nguo aliyokuwa anatumia kulalia.

Kifo chake kimeibua maswali mengi kwa watu mbalimbali wakiwemo wanaharakati, huku Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch likitaka uchunguzi ufanyike kuhusu kifo hicho.

Mkurugenzi wa shirika hilo katika kanda ya Afrika ya kati, Lewis Mudge, ameliambia shirika la Habari BBC, kuwa shirika hilo linatilia shaka mazingira ya kifo chake na kwamba linataka uchunguzi huru ufanywe.

Mudge ameongeza kuwa Kizito Mihigo alikuwa mwakilisha watu wanaojaribu kushinikiza mabadiliko nchi Rwanda miaka 26 baada ya mauaji ya kimbari.

''Hii sio mara ya kwanza watu kufariki wakiwa kizuizini au kuawa katika mazingira ya kutatanisha au kutoweka'' alisema Bw. Mudge akifafanua kauli yake.

Ameongezea kuwa mwaka 2018 mwanasiasa maarufu wa upinzani alitoweka akiwa jela na kwamba mamlaka ya jela wakati huo zilisema mwanasiasa huyo alikuwa akijaribu kutoroka lakini tangu wakati huo hajawahi kupatikana.

Kizito Mihigo ni nani?

Mihigo aliyekufa akiwa na miaka 34, mbali ya kuwa mwanamuziki wa Injili, pia ni mwanaharakati, alijizolea umaarufu kutokana na kuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Paul Kagame kupitia sanaa yake.

Mwaka 2015 alihukumiwa miaka 10 gerezani kutokana na kuimba nyimbo za kuhamasisha raia kudai haki ambapo mamlaka zilidai kwa anachochea vurugu na kuhatarisha amani.

Kutokana na tuhuma hizo alikamatwa na kuhukumiwa miaka 10 ambapo kati ya hiyo alitumikia miaka mitatu na mwaka 2018 akaachiwa kwa msamaha wa Rais.

Aliporudi mtaani akaendelea na kazi zake za uimbaji za kumuabudu na kumtukuza Mungu na pia kuendelea kupigania haki na usawa miongoni mwa Wanyarwanda ikiwemo vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na vyombo vya dola, akitetea haki za binadamu na utawala bora.