Kiongozi wa kanisa aomba radhi kwa corona kusambaa

Muktasari:

  • Muumini wake alipata homa na kuhudhuria ibada kwa siku nne jijini Daegu ambako virusi vya corona viliibukia Korea Kusini.

Kiongozi wa kiimani wa kikundi kinachohusishwa na nusu ya maambukizi 4,000 ya virusi vipya vya corona, amepiga magoti mbele ya kamera na kuomba radhi kutokana na kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa huo.

Maombi ya Shincheonji, kiongozi wa Lee Man-hee, yamekuja baada ya mamlaka ya jiji la Seoul kufungua kesi ya mauaji dhidi yake kutokana na kushindwa kutoa ushirikiano kuukabili ugonjwa huo unaosababisha mafua na joto la mwili kupanda.

Idadi ya maambukizi nchini Korea Kusini ambayo ni kubwa kuliko sehemu nyingine yoyote nje ya China inatarajiwa kuongezeka wakati mamlaka zikikagua zaidi ya watu 266,000 wanaohusishwa na Kanisa la Yesu la Shincheonji.

"Napenda kuomba radhi kwa dhati kwa wananchi," alisema Lee kwa sauti inayokatikatika.

"Ingawa haikuwa makusudi, watu wengi wameambukizwa," alisema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 88, akiinamisha kichwa chake chini mara mbili mbele ya waandishi wa habari.

"Naomba radhi kwa watu."

"Naishukuru serikali kwa juhudi zake," alisema. "Pia naiomba radhi serikali."

Lee anachukuliwa na waumini wake kama kiongozi aliyeahidiwa kuja ambaye amechukua mafundisho ya Yesu Kristo na ataondoka na watu 144,000 kwenda nao mbinguni siku ya hukumu.

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 61 alipata homa Februari 10 lakini akahudhuria ibada nne mjini Daegu -- mji wa nne kwa ukubwa nchini Korea Kusini na ambao una watu milioni 2.5 na ambako maambukizi hayo yalianzia -- kabla ya kugundulika ana maambukizi ya virusi hivyo.

Wakati wa ibada, waumini hao wa Shincheonji hukaa karibu pamoja na kuomba kwa nguvu, mazingira ambayo wakosoaji wanasema yanachangia kuambukiza ugonjwa huo.

Lee ambaye anasema waumini wa kanisa lake hawajaambukizwa virusi hivyo alisisitiza kuwa kundi lake limeshirikiana na serikali.

"Katika makanisa, kiongozi wa kanisa ni kama mzazi na waumini wake ni watoto," alisema, akitulia kila wakati kufuta machozi huku waandamanaji wakipiga kelele kusema kuwa anatumia vibaya imani.

"Wazazi gani watasimama na kuangalia wakati kuna ugonjwa kama huu ambao unaweza kusababisha kifo?"