Mahakama yamtia hatiani Ntaganda

Muktasari:

Ntanganda maarufu Terminator amekutwa na hatia katika makosa 18 ikiwamo mauaji, ubakaji, utumwa wa kingono na kuwatumikisha watoto wadogo katika jeshi

The Hague, Uswisi. Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC mjini The Hague imemtia hatiani kiongozi wa waasisi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Bosco Ntaganda kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Kwa zaidi ya miaka mitatu Ntaganda alikuwa akikabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita anaodaiwa kufanya nchini Congo.

Jaji, Robert Fremr alisema mahakamani hapo leo Jumatatu Julai 8,  kuwa Ntanganda maarufu Terminator amekutwa na hatia katika makosa 18 ikiwamo mauaji, ubakaji, utumwa wa kingono na kuwatumikisha watoto wadogo katika jeshi.

Ntaganda mwenye umri wa miaka 45 alishtakiwa kwa kusimamia mauaji ya raia na wanajeshi wake katika eneo linalokabiliwa na machafuko na lenye utajiri wa madini la Ituri Mashariki mwa Congo mwaka 2002 na 2003.

Sehemu ya ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo unadai kuwa kiongozi huyo alikuwa akiwakata koromeo na kisha kutoa viungo vya ndani, kuchinja watu na kuwa kufanya utumwa wa kingono.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa pia Ntaganda alishirikiana na waasi wakati wa vita vilivyoiyumbisha Congo baada ya mauaji ya halaiki ya 1994 katika Taifa la Rwanda.

Kwa mujibu wa Shirika la Kutetea haki za binadamu, watu zaidi ya 60,000 waliuawa tangu machafuko hayo yalipozuka katika eneo hilo mwaka 1999 wakati waasi wapipokabiliana kupigania udhibiti wa raslimali ya madini.

Ilidaiwa kuwa Ntaganda pia alishiriki katika vuguvugu la M23, ambalo lilisaini mkataba wa amani na Serikali ya Congo mwaka 2013.

Hata hivyo, alijisalimisha mwenyewe kwa ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali mwaka 2013 baada ya kuepuka mitego ya kumkamata kwa miaka saba.