Maisha ya Nikita kuishi na saratani ya ubongo kwa miaka 15

Muktasari:

Msanii wa filamu nchini Uganda, Nikita Pearl Waligwa ambaye alikuwa anafahamika kwa jina la Gloria katika filamu ya Queen of Katwe. Aliigiza filamu hiyo kwa ucheshi na bashasha huku akikabiliwa na tatizo la saratani ya ubongo.

Uganda: Licha ya kuwa na tatizo la saratani ya ubongo kwa muda mrefu, nyota wa filamu ya ‘Queen of Katwe’, Nikita Pearl Waligwa ,haikuwa tatizo kwake kuonyesha kipaji cha kuigiza alichonacho.

Nikita aliyekuwa na umri wa miaka 15, aliigiza filamu mbalimbali nchini humo, lakini alipata umaarufu zaidi pale alipoigiza na mwigizaji maarufu duniani mwenye asili ya Kenya, Lupita Nyong'o.

Katika filamu hiyo ya Queen of Katwe, msanii huyu aliigiza kama mtoto wa mshindi wa tuzo ya Grammy Lupita na mwalimu wa mchezo wa chess, filamu ambayo iliweza kufanya vizuri ndani na nje ya Uganda.

Katika filamu hiyo ya mwaka 2016 inayotokana na hadithi ya kweli ya Phiona Mutesi , nyota wa mchezo wa chess kutoka mtandao mmoja wa mabanda nchini Uganda.

Mwaka huohuo wa 2016 ndio Waligwa kwa mara ya kwanza aligundulika kuwa na uvimbe katika ubongo ambapo mkurugenzi wa filamu ya Queen of Katwe , Mira Nair aliripotiwa kutuma watu ili kusaidia kufadhili matibabu yake nchini India baada ya madaktari wa Uganda kueleza kuwa hawakuwa na vifaa vinavyoweza kumtibu.

Wahisani mbalimbali walijitokeza kumsaidia na kutibiwa tatizo hilo ambapo  mwaka 2017 alikaa sawa na kurudi kuendelea na masomo yake katika shule ya Sekondari Gayaza alipokuwa akisoma.

Hata hivyo ilipofika mwaka jana 2019 aligundulika tena kuwa na uvimbe mwingine katika ubongo ambapo alikuwa amelazwa katika hospitali moja nchini Uganda ambapo familia iliomba msaada wa Sh73 milioni kwa ajili ya kumpeleka nchini India.

Kwa bahati mbaya fedha hiyo haikupatikana  mpaka pale umauti ilipomkuta mtoto huyo.

Kifo chake kilitangazwa na shule kupitia mtandao wa twitter kwa kuandika ''Ulikuwa kipenzi cha wengi na sasa tumekupoteza kupitia saratani ya ubongo katika umri mdogo'', ilisema shule ya upili ya Gayaza.

 

Nyota mbalimbali alioshiriki kucheza nao akiwemo David Oyelowo, walionyesha masikitiko yao kuhusiana na msiba huo mzito kwao kwa kuandika katika kurasa zao kwenye mtandao wa Instagram.  ‘Alikuwa mwangaza katika Queen of Katwe na maishani’.

Lupita aliandika “Aliigiza kama Gloria na uwezo mkubwa . Katika maisha yake alikuwa anakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na saratani ya ubongo.

Huku Gloria Nansubuga, kijana wa miaka 19 kutoka Uganda ambaye ni nyota wa mchezo wa chess ambaye ndiye alimuigiza katika filamu hiyo, aliambia BBC,  “Siwezi kuhimili habari kwamba mtu aliyeniigiza katika filamu amefariki.

 

''Nampenda kutoka moyoni mwangu. Aliniambia kwamba alitaka kujifunza kucheza chess . Nilitaka kuwa na mafunzo naye lakini alikuwa hospitali kila mara,  Alikuwa mkarimu licha ya kuwa na umri mdogo''.

Inaelezwa kuwa nchini Uganda ni kiwango kidogo cha wagonjwa walio na hali mbaya kama hiyo ya Nikita ambao hupata usaidizi huo wa kimatibabu kutokana na gharama za matibabu yake kuwa juu.

Moja ya mambo ambayo yatakumbukwa kwa Nikita  ni usemi wake aliopenda kuutumia kuwa ‘siku moja ndogo inaweza kuja kuwa kubwa’ kauli mbiu iliyotumika pia wakati wa hafla ya uzinduzi wa filamu hiyo ya Queen of Katwe uliofanyika mwaka 2018 nchini Uganda ambapo watu walikuwa wakimsalimia kila walipomuona kwa usemi huo.