Mambo yazidi kuwa mabaya kwa Kardinali mbakaji

Muktasari:

Mahakama Kuu nchini Australia imedhibitisha hukumu ya kuwalawiti watoto na kutupa rufaa yake.

Australia. Mahakama Kuu nchini Australia imetupa rufaa ya kupinga hukumu ya miaka sita kwa Kardinali wa Kanisa Katoliki, George Pell.

Kardinali Pell alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwalawiti watoto wawili wa kiume.

Kardinali Pell alirejeshwa gerezani leo Jumatano Agosti 21 ambako ataendelea kutumikia kifungo chake cha miaka sita kwa kuwashambulia kingono wavulana wawili wenye umri wa miaka 13 waliokuwa wanaimba kwaya kwenye kanisa mjini Melbourne katika miaka ya 1990.

Pell mwenye umri wa miaka 78 alikuwa amevaa suti nyeusi na mara kwa mara alikuwa akiinamisha kichwa chake wakati Jaji Mkuu, Anne Ferguson akisoma hukumu yake huku kundi la watu lililokusanyika nje ya mahakama hiyo likishangilia.

Jaji Ferguson alisema kutokana na uamuzi huo sasa Kardinali Pell atastahili kupewa msamaha baada ya kutumikia gerezani kwa miaka mitatu na miezi minane.

Hata hivyo, Jaji Ferguson alisema endapo Kardinali Pell hakuridhika na uamuzi huo anaweza kuiomba mahakama ya juu zaidi kusikiliza rufaa yake.

Katika rufaa hiyo wakili wa Kardinali Pell waliainisha vipingamizi 13 na kutilia mashaka uwezekano wa kimwili wa Pell kuvua majojo yake kumbaka mvulana hadi kwenye uaminifu wa shahidi mkuu.

Pell ndiye kiongozi wa juu zaidi wa Kikatoliki kutiwa hatiani kwa makosa ya udhalilishaji wa watoto kingono.