Matumizi ya noti ya Sh1,000 mwisho leo Kenya

Muktasari:

Juni mwaka huu Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitangaza matumizi ya noti hizo na kutoa miezi minne kwa wananchi wote kubabadilisha sarafu hiyo.

Nairobi, Kenya. Leo ni siku ya mwisho wa matumizi ya noti ya zamani ya shilingi 1,000 nchini Kenya.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mara baada ya kufutwa kwa noti hiyo Serikali kupitia Wizara ya Fedha itatangaza hatua nyingine  ya mabadiliko katika sarafu nyingine kwa awamu.

Juni mwaka huu Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitangaza matumizi ya noti hizo na kutoa miezi minne kwa wananchi wote kuhakikisha wanabadilisha sarafu hiyo.

Gavana wa Benki Kuu, Patrick Njoroge alisema operesheni hiyo ililenga kukabiliana na ufisadi na mtiririko wa fedha haramu ambazo alikiri kukithiri nchini humo.

Ubunifu wa sarafu mpya, ambayo ina mfano wa sanamu ya Rais wa kwanza wa Kenya na baba Rais wa sasa, Jomo Kenyatta umesababisha hasira kwa baadhi ya Wakenya.

Mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka nchini humo walifungua kesi Mahakamani na kudai kuwa kutumika kwa picha ya Rais huyo wa zamani ni kinyume cha Katiba ambayo inakataza matumizi ya picha za watu kwa sarafu yoyote.

Hata hivyo, Mahakama Kuu nchi humo wiki iliyopita ilitupilia mbali shauri hilo na kusema kuwa noti hiyo ilitumia sanamu Rais  huyo wa zamani Mzee Kenyatta na haikuwa picha.

Mahakama hiyo pia ilikataa kuongeza tarehe ya kumalizika kwa noti za zamani za Sh1,000 uliowekwa na Serikali.

Tangazo la Rais Kenyatta

Mapema Juni mwaka huu, Rais Kenyatta alitangaza kwamba sarafu ya nchi hiyo inapaswa kubadilishwa na kizazi kipya cha noti.

Rais Kenyatta alitoa tarehe ya mwisho kwa Wakenya kurudisha noti hiyo ya Sh1,000 katika benki kabla ya Oktoba Mosi.

Alisema lengo la mpango huo ni kupambana na utapeli wa fedha bandia na ufisadi na kuongeza kuwa machapisho mapya yataletwa miezi ijayo na sarafu nyingine zitatolewa pole pole.

Hatua ya Rais Kenyatta inaelezwa kuwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2013 kwamba atahakikisha anamaliza ufisadi katika nchi hiyo.

Lakini wakosoaji wake wanasema kumekuwa na matumaini madogo juu ya kumaliza ufisadi huo hasa kwa watu wa hali ya juu.

Mwandishi wa biashara wa BBC Africa, Georgie Ndirangu anasema uondoaji wa sarafu na noti hizo utapunguza vitendo vya kifisadi vilivyokuwa vimeshamiri katika nchi hiyo.