Mwafrika wa kwanza apona corona, alitumia ARV

Muktasari:

Kem Senou Pavel Daryl ni mwafrika wa kwanza kuambukizwa virusi vya corona chini China.

Guangzhou, China. Mwanafunzi raia wa Cameron amesimulia jinsi dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi zilivyomponya corona (covid-19).

Aidha, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 aliyeambukizwa virusi hivyo nchini China alisema katika kipindi chote cha matibabu yake yaliyodumu kwa siku 13 alikuwa akipewa dawa za antibiotiki na na ARV.

Kem Senou Pavel Daryl anayeishi katika mji wa Guangzhou alisema alianza kupata homa kali, kukohoa vibaya na kuonyesha dalili za mafua na baada ya vipimo aligundulika kuambukizwa virusi vya corona.

Akisimulia mkasa huyo, mwanafunzi huyo alisema ingawa alikuwa katika maumivu makali hakuwa na mpango wa kuondoka China hata kama hilo lingewezekana.

“Niliwaza sana, chochote kitakachofanyika sitaki kupeleka ugonjwa Afrika,” alisema mwanafunzi huyo akiwa katika chumba eneo maalumu alilotengwa kwa siku 14 sasa.

Alisema alipokuwa akieenda hosipitali kwa mara ya kwanza aliona kifo lakini baada ya kupewa dawa za kutibu wagonjwa walio na virusi vya ukimwi na antibiotic kwa wiki mbili alianza kuonesha dalili ya kupona.

Pavel Daryl ni mtu wa kwanza mwenye asili ya Afrika aliyepona baada ya kuambukizwa na virusi hatari vya corona ambako sasa umeingia barani Afrika. Misri ni nchi ya kwanza kuthibitisha kisa cha maambukizi ya virusi vya corona.

Wataalamu wa Afya wameonya kuwa nchi zlizo na mifumo hafifu za matibabu huenda zikakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo ambavyo mpaka sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,600 na wengine 68,000 kuambukizwa.