Polisi Ecuador wakusanya mitaani maiti 800 za waliofariki kwa corona

Muktasari:

  • Uamuzi wa polisi na wanajeshi kukusanya maiti mitaani ulitokana na wakazi kutuma picha mitandaoni wakitaka ndugu wa familia wasaidiwe kuzika.

Ecuador imesema polisi wameondoa karibu miili 800 katika wiki za karibuni kutoka katika makazi mjini Guayaquil, sehemu iliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa virusi vya corona, baada ya ugonjwa huo kuzidi uwezo wa huduma za dharura, hospitali na kampuni za mazishi.


Wafanyakazi katika vyumba vya kuhifadhia maiti katika mji huo wa pwani wamekuwa wakishindwa kukabiliana na vifo, huku wakazi wakituma video katika mitandao ya kijamii zinazoonyesha miili iliyotelekezwa mitaani


"Idadi ya miili tuliyokusanya pamoja na kikosi maalum kutoka katika makazi inazidi maiti 700," alisema Jorge Wated, ambaye anaiongoza timu ya polisi na wanajeshi iliyoundwa na serikali kusaidia kukabiliana na athari za ugonjwa wa Covid-19.


Baadaye alisema katika akaunti ya Twitter kwamba kikosi hicho cha pamoja, kilikusanya miili 771 kutoka katika nyumba za wakazi na mingine 631 kutoka hospitalini ambakovyumba vya kuhifadhia maiti vimejaa.


Wated hakueleza sababu ya vifo vya watu hao, ambao 600 wamezikwa na mamlaka.


Ecuador imetangaza kugundua maambukizi kwa watu 7,500 tangu ilipothibitisha mtu wa kwanza Februari 29.
Jimbo la pwani la Guayas lina asilimia 70 ya maambukizi yote, huku watu 4,000 walioambukizwa wakiwa wanatoka Guayaquil, kwa mujibu wa taarifa z aserikali.


Wanajeshi na polisi walianza kuondoa miili hiyo wiki tatu zilizopita baada ya mfumo katika vyumba vya kuhifadhia maiti mjini Guayaquil kuharibika, na hivyo kusababisha ucheleweshaji katika huduma za uchunguzi na mazishi.


Wakazi wa Guayaquil walituma mitandaoni picha za miili iliyotelekezwa mitaani pamoja na ujumbe unaotaka ndugu wa familia wasaidiwe kuzika.


Serikali ya Ecuador imechukua jukumu la kuizika miili hiyo, kutokana na ndugu kutokuwa na uwezo wa kuzika kwa sababu tofauti, ikiwemo ya kifedha.