R Kelly ahofia virusi vya corona akiwa gerezani, ataka aachiwe huru

Mwimbaji wa muziki wa R&B, R Kelly amemuomba jaji kumuachia huru kutoka katika Gereza la Chicago akihofia kupata maambukizi ya ugonjwa wa corona au Covid-19.

Hivi karibuni majaji wa mahakama za Chicago walionyesha nia ya kumuachia kwa dhamana msanii huyo, lakini jaji wa New York akasema abaki gerezani.

Robert Kelly maarufu R. Kelly amekuwa akikamatwa mara kadhaa. Mapema Julai, 2019 alikamatwa kwa mara ya pili na Idara ya Polisi ya New York kwa tuhuma za kuwasafirisha wanawake kwa ajili ya kuwatumikisha kingono.

Mara ya kwanza alikamatwa Februari mwaka jana kwa tuhuma za kuhusika na makosa 10 ya ngono.

Mei alikamatwa tena na kushtakiwa kwa tuhuma za kuhusika na makosa 11 ukiachilia makosa 13 ya awali ya unyanyasaji wa kingono ambapo kati ya makosa hayo yalikuwemo yanayohusisha kifungo cha hadi miaka 30 jela.

Kwa mujibu wa tovuti ya CNN, imeeleza kuwa barua ya maombi hayo iliwasilishwa mahakamani hapo na wakili wake Steven Greenberg ilieleza namba mteja wake huyo mwenye miaka 53 yupo katika hatari ya kupata maambuziki hayo.

Barua hiyo ilieleza namna katika gereza la Metropolitan Correctional Center kusivyokuwa na sabuni na sanitaiza za kutosha na watu wengi wanawekwa katika selo ndogo mbili na kuwapo na msongamano ambao ni hatari kipindi hiki.

“Katika vyoo na mabafu vya wageni hapa MCC, hakuna sabuni wala karatasi laini za msalani, hivyo inakuwa ngumu kuosha mikono kabla ya kuingia ndani kuona wafungwa na mahabusu”ilisema sehemu ya barua hiyo.

Katika kesi hizo mwimbaji huyo anatakiwa kuripoti mahakamani siku na miji tofauti, ambapo Julai mwaka huu anatakiwa New York, huku Oktoba 13 akitakiwa Chicago.